June 15, 2015


Na Saleh Ally
BODI ya Ligi imetumia wataalamu wake kudadavua mambo kadhaa hadi kufikia kuwatangaza wachezaji na makocha bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.


Moja ya mambo ambayo yaliwashangaza wengi lilikuwa ni lile la Kocha Mbwana Makata wa Prisons kuwa Kocha Bora wa Msimu wa 2014-15.

Makata ametangazwa kuwa kocha bora wa msimu baada ya kushiriki mechi tisa tu. Kati ya hizo amefanikiwa kushinda nne, sare nne na kupoteza moja.

Katika mechi tisa, Makata alikusanya pointi 16 na kuisaidia Prisons kuepuka kuporomoka daraja na kuiwezesha Mbeya kubaki na timu mbili katika Ligi Kuu Bara.

Makata amekuwa kocha bora baada ya kuwashinda makocha wawili wageni, Goran Kopunovic wa Simba aliyeiwezesha timu yake kushika nafasi ya tatu na Hans van Der Pluijm aliyeipa Yanga ubingwa.

Ukiiangalia rekodi ya Makata ya mechi tisa na kukusanya pointi 16, akiwa ameshinda mechi tatu na sare mbili nyumbani, amepoteza moja, sare moja na kushinda moja akiwa ugenini, bado haitoshi kumpa nafasi ya kuwa kocha bora.
MALINZI NATIMU YAKE YA TFF; WASIIACHIE BODI YA LIGI IFANYE INAVYOTAKA.

Kaiokoa timu kuteremka daraja, sawa. Lakini kuna kocha aliyeipa timu ubingwa, kuna kocha aliyeipa timu nafasi ya tatu na zote zilikuwa katika hali mbaya.

Kopunovic aliichukua Simba ikiwa taabani kutoka kwa Phiri, akaibadilisha, ikaanza kuonyesha soka la kuvutia na kihesabu inaonekana ndiyo timu iliyofanya vizuri zaidi katika mzunguko wa pili kuliko nyingine zote.

Simba ni kati ya timu zilizofungwa mabao machache zaidi na tuliona hata soka lake lilikuwa ni la kuvutia. Hivyo kocha anayeonekana kuwa na ubora kati ya Makata na Mserbia huyo, jibu liko wazi kabisa.

Ukirudi kwa Pluijm, unakumbuka wakati anaichukua timu kutoka kwa Marcio Maximo. Ilionekana iko taabani, uchezaji wake wa kubahatisha, lakini kafanya mabadiliko makubwa.
Mwisho Yanga imekuwa ni ya uhakika na tishio, imemaliza msimu ikiwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi, iliyofungwa machache zaidi na ndiyo mabingwa.

Sasa kocha aliyeisaidia timu kutoshuka daraja inawezekana vipi akawa bora kuliko huyo? Ukiangalia wastani wa ushindi, sare na kupoteza kati ya makocha hao watatu, ule wa Makata unaonekana uko chini.

Mechi tisa kapoteza moja. Nane zilizobaki kazigawa kwa sare na ushindi. Ushindi wa zaidi ya mechi kumi kutoka kwa Pluijm, vipi awe chini ya Makata?

Ukiangalia unaona kuwa uteuzi umefanyika kwa kuangalia mambo mawili. Moja inawezekana ni imani ya uzalendo au kutaka ‘kubalansi’ mambo na fulani apate.

Kwamba huyu ni mzalendo mwenzetu, kwa nini tuwape Wazungu tu? Au tuzo zote watachukua na Simba pekee, basi tuangalie na timu nyingine ili ‘kubalansi’ na kuwapa nguvu, kosa kubwa.

Iko haja ya kumuacha kila mmoja asimame kwa miguu yake. Kuwapa wazalendo tuzo wasizostahili, ni kuwadanganya na kuzidi kuwadumaza.

 Pili ni suala ambalo nimelisikia. Kwamba hakukuwa na watu imara kwa maana ya utaalamu waliofanya kazi hiyo ya uteuzi. Lakini kati ya wajumbe, baadhi walikuwa na mchezo mchafu wa kuzigeuza tuzo hizo kuwa mradi wa kujifaidisha kwa kuwa wadhamini walikuwa wanatoa zawadi za fedha.

Kuna mchezaji mmoja amelalamika kwamba kwa kuwa yuko katika kundi la wale wanaogombea, basi alipigiwa simu na kuambiwa afanyiwe mpango wa kushinda moja ya kipengele halafu fedha atagawana na mhusika na wenzake.

Nimeambiwa kazi ya uteuzi wa wajumbe na upatikanaji wa washindi ilifanywa na watu wa Bodi ya Ligi. Huenda wapo waliokuwa na nia nzuri, lakini kuteua kwa kutozingatia vigezo kumekuwa tatizo kwa kuwa wapo wanaotaka kujifaidisha wao, matumbo yao na familia zao na si mpira wa Tanzania.

Hivyo wanaona, mchezaji anayekubali kugawana zawadi yake, ndiyo anakuwa na nafasi ya kupata ushindi bila ya kuangalia kama ni sahihi au la.

Sitaki kwenda mbali kuhusiana na ushindi wa wengine. Huu wa Makata kwangu ulikuwa ni mfano tosha kwamba kuna madudu ndani ya kazi hii ya utoaji tuzo.

Kama itaendelea, mwisho itapoteza maana na wenyeji au wazalendo watakuwa wakidanganyika kwa ubora usio sahihi.
Wale wanaotaka kuzigeuza tuzo hizo kama mtaji au mradi, wanapaswa kubadilika na kujua wanachafua mbio za maendeleo ya mpira wa Tanzania.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lina dhamana kubwa katika suala la heshima ya Tanzania. Hata kama Bodi ya Ligi Tanzania ndiyo wahusika. Basi kuna wakati linapaswa kusimamia ubora wa mambo yanayoweza kuvuruga heshima ya soka Tanzania. Hili ni mfano na Jamal Malinzi na timu yake wafungue macho.

MBWANA MAKATA AMEIONGOZA PRISONS MECHI 9
SHINDA 4
SARE 4
POTEZA 1

Machi 14, 2015

Prisons                      3-0                  Stand                                    Sokoine
Laurian Mpalile 30
Salum Kimenya 65
Hamis Maigo


Machi 22, 2015
Prisons          0-0                  Polisi Moro              Sokoine


Aprili 4, 2015
Coastal          0-1      Prisons                      Mkwakwani
                                    Jeremiah Juma 44


Aprili 11, 2015
Ndanda        0-0      Prisons                      Nangwanda


Aprili 15, 2015
Mtibwa         1-0      Prisons                      Jamhuri

Aprili 19, 2015
Prisons          1-1                  Mtibwa                     Sokoine
Lugano Mwangama 77     Mgosi 40

Aprili 26, 2015
Prisons          2-0                  Mgambo      Sokoine
Fred Chudu 16
Boniface Hau 87

Mei 2, 2015
Prisons          1-0                  Mbeya                      Sokoine
Lugano Mwangama 90 (penalti)

Mei 9, 2015
Kagera          0-0                  Prisons                      Kaitaba
Fin.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic