Mbiombio za mazoezi ya Yanga si mchezo na kipa namba moja wa timu
hiyo, Ally Mustapha ‘Barthez’, anaweza kuwa shahidi wa hilo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, anaonyesha
hataki mchezo maana alimkimbiza Barthez hadi akaomba “po”.
Timu hiyo ilianza mazoezi ya pamoja juzi Jumanne kwa ajili ya
kujiandaa na Michuano ya Kombe la Kagame iliyopangwa kuanza Julai, mwaka huu.
Kipa huyo aliripoti kwenye mazoezi hayo jana Alhamisi na kukutana
na msoto wa mbio ndefu zilizoongozwa na Pluijm akisaidiwa na Charles Mkwasa.
Wakati akiendelea kukimbia mbio hizo, kipa huyo alishindwa
kuendana na kasi ya wachezaji wenzake aliowakuta baada ya kuishiwa na pumzi
katikati ya mazoezi.
Kipa huyo alionekana kuchoka wakati wenzake wakifuata programu ya
kocha huyo ya kuzunguka uwanja baada ya wakati wote kuwa wa mwisho wakiwa wanakimbia.
Barthez alichoka wakiwa katika raundi ya 25 ya kuzunguka uwanjani
hapo na ndiyo akamuomba kocha wake kupumzika na alipokubaliwa akalala chali na
kuonekana kama mtu aliyepoteza ‘network’.
Kuona hivyo, Pluijm alimtaka Daktari Mkuu wa Yanga, Juma Sufiani
kumfuata Barthez kwa ajili ya kumuangalia ambaye alifika na kumnyoosha mwili na
baadaye kuendelea na programu nyingine ya mazoezi.
Alipoulizwa Barthez kuhusiana na hali hiyo, alisema: “Kiukweli
kabisa pumzi ziliniishia wakati tunakimbia, ndiyo maana nikamuomba kocha
nipumzike kwanza.
“Ujue tangu ligi kuu ilipomalizika sikufanya mazoezi ya nguvu,
zaidi nilikuwa ninafanya mazoezi madogomadogo, lakini siyo kama haya
niliyoyakuta hapa.”








0 COMMENTS:
Post a Comment