| PAZI WAKATI SIMBA... |
Uongozi wa Mwadui FC umefanikiwa kunasa saini ya aliyewahi kuwa kiungo
wa Simba, Zahoro Pazi ambaye ndiye aliyefunga usajili wa timu hiyo huku
ukimuajiri Habibu Kondo kuwa kocha msaidizi wa kikosi hicho akishirikiana na Kocha
Mkuu, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Zahoro aliondoka Simba baada ya msimu wa 2013/14 akaelekea FC
Lupopo ya DR Congo ambayo hata hivyo hakuichezea kutokana na kukosa Hati ya
Uhamisho wa Kimataifa (ITC), ikamlazimu arudi Bongo, akatua Polisi Moro ambayo hakuichezea
kutokana na kukuta dirisha la usajili limefungwa. Baada ya kushindwa kucheza
msimu wote uliopita, sasa ametua Mwadui FC.
Hadi sasa, kikosi hicho kimefanikiwa kusajili nyota wapatao kumi kutoka
klabu tofauti huku kikiwaongezea mikataba wachezaji 13 walioipandisha timu.
Katibu wa Mwadui FC, Ramadhan Kilao amesema kwa sasa baada ya
kumsajili kiungo huyo, hawataongeza mchezaji mwingine.
Alisema tayari nyota wao wapo kambini kwa ajili ya kuanza mazoezi
huku akiahidi watasumbua sana msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
“Leo tumefanikiwa kumalizana na kiungo Zahoro Pazzi ambaye
amesaini mkataba wa mwaka mmoja, pamoja na Kocha Habibu Kondo aliyechukua
nafasi ya Amri Said,” alisema Kilao.







0 COMMENTS:
Post a Comment