June 12, 2015


Na Saleh Ally
MABINGWA wa soka Tanzania, Yanga wamewasilisha barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ni wenyeji wa michuano ya Kombe la Kagame kwamba wanapinga kabisa wapinzani wao wakubwa Simba, kushiriki.


Michuano ya Kagame imepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam, taarifa zinaeleza kuanzia Julai 11.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cefaca), liliamua Simba washiriki kama waalikwa ili kuamsha hamasa zaidi ya mashabiki kutokana na ukubwa wa kikosi cha Simba.

Simba ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo hivyo ndivyo vigezo viwili walivyovitumia Cecafa kuialika Simba.

Yanga wameona hapana, wanadai kwamba wao ndiyo wenye haki, hawakubaliani na hilo. Hapo kuna jambo ambalo hawajaliweka wazi ingawa linaeleweka, kwamba Yanga wana hofu ya Simba.

Wanapaswa kuwa na hofu, lakini ingekuwa vizuri wasionyeshe uoga wa aina hiyo. Wanajua wakikutana na Simba, basi wako matatizoni. Huenda ingekuwa vizuri wajipime kwa mara nyingine.

Kwa upande wa Cecafa tunajua, pamoja na kutumia vigezo viwili kuwa Simba ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, timu itayosaidia kuchangamsha michuano hiyo. Lakini ukweli ni kwamba wanataka mapato zaidi na wanajua kama ilivyo kwa Yanga, Simba nayo ina watu wake.

Wanachoangalia Cecafa ni kuchangamka kwa mashindano lakini ukweli hasa ni hilo la mapato. Sasa Yanga hawataki!

Kukataa kwa Yanga, kunaweza kukawavuruga Simba na kuona kama wananyimwa haki ya kushiriki kutokana na hofu ya Yanga kwao. Mimi ninaona ikiwezekana, Simba wanapaswa kuwashukuru wapinzani wao hao.

Wanapaswa kuwashukuru kwa kuwa kikosi cha Simba hakihitaji mashindano kama ya Kagame katika kipindi hiki. Badala yake wanahitaji kambi ya pre season ya kutosha tena iliyokamilika kweli.

Simba inahitaji kambi tulivu, inahitaji kwenda kujichimbia ikiwezekana kwa ajili ya kuunda kikosi upya. Kutengeneza timu ikiwa na baadhi ya wachezaji wapya na kocha mpya.
Kocha mpya wa Simba anapaswa kukiona kikosi chake, kufanya mazoezi ya kutosha na kama ni mechi, zitafuata baada ya kikosi kuwa kimeiva kwa maana ya ‘fitness’.

Mara nyingi timu nyingi za Tanzania zimekuwa zikiingia katika janga la majeraha kutokana na wakati mbaya kama huo wa michuano ya Kagame. Wakati inakuja kufanyika nchini, baadhi ya timu za nchi kama Rwanda, Kenya wanakuwa ndiyo wanatoka kwenye ligi, maana yake wako fiti.

Wachezaji wa timu za Tanzania, wengi wanakuwa si fiti kwa vile ligi imeisha kitambo na wanapata muda mchache wa kufanya mazoezi magumu na ya kutosha ili kujiweka sawa.

Kawaida angalau wiki nne hadi sita, wachezaji wanapaswa kufanya mazoezi magumu. Baada ya hapo taratibu wanapunguza ugumu wa mazoezi na kuchezea mpira zaidi. Ndiyo kipindi ambacho angalau mechi za kirafiki zinaingia.

Ukiangalia Simba itakuwa na muda kiasi gani wa kujiandaa. Kipindi cha muda upi wa kutosha hadi kocha mpya awe amekiona kikosi chake na kuanza kukipanga kwa ajili ya michuano, tena ya kimataifa.

Simba inaweza kushindwa kuonyesha cheche zake na kocha akaonekana hana lolote, kumbe tatizo likawa ni haraka ya kushiriki michuano hiyo.

Lakini kwa kuwa wachezaji hawako fiti, Simba inaweza kuingia katika kusababisha baadhi ya wachezaji wake kuumia na wakati mwingine wakawa ‘vimeo’ msimu wote na kuifanya iwakose kwa kushindwa kuwatumia kwa asilimia mia kutokana na kuwa majeruhi.

Kuna kila sababu ya kujipima mara mbili kwa Simba kabla ya kuingia katika michuano hiyo. Huenda kutaka mashabiki waione timu au kupata fedha kidogo linaweza kuwa lengo namna moja.

Bado iko haja ya kuangalia kama lengo hilo lina faida na hasara zake ni zipi hapo baadaye. Siwezi kuizuia Simba kuingia na kushiriki, lakini uongizi utafakari mara mbili katika hili. Kwani furaha ya wiki mbili kwa mashabiki, bado haiwezi kulingana na ile ya msimu mzima kama timi itaandaliwa vizuri kwa kufuata misingi sahihi.

Bado uongozi wa Simba unaweza kuwa unatamani kuitumia michuano hii kujiingizia kipato. Lakini lazima iangalie hasara inayoweza kupata kwa msimu mzima.

Siwezi kuwa rais wa klabu hiyo, lakini ningeipata nafasi hiyo angalau kwa dakika tano tu, basi uamuzi wa kwanza ulikuwa ni kutamka hivi; “Simba haitashiriki michuano ya Kagame”.



1 COMMENTS:

  1. pre-season matches ok hawanabudi simba kutafuta nakucheza ili kuwaweka sawa kwasababu watakuwa na wachezaji pamoja na kocha mpya.kwa hili lawachezaji kuumia kuwa majeruhi kama watashiriki kagame hapana,mchezaji anaweza kuumia hata mazoezini.simba wakipata washiriki.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic