BARCELONA ndiyo mabingwa wapya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, hiyo siyo
habari mpya kwa sasa lakini habari ni kuwa kwa nini Barcelona?
Wapo ambao wamekuwa wakimtazama Lionel Messi kuwa ndiye nguzo muhimu
kwa timu hiyo kutwaa mataji matatu msimu huu, hilo ni kweli lakini hali halisi
ni kuwa Barcelona imeshinda taji hilo kwa kuwa kila mtu kwenye timu kafanya
kazi yake vizuri.
Messi amekuwa akionekana zaidi kwa kuwa uwezo wake ni wa kipekee na
amekuwa akionyesha makubwa zaidi hata ya wenzake lakini baada ya kuanza msimu
kwa kuyumba, hatimaye Barcelona ilianza kuelewana na kufanya kila mtu kucheza
kwa kiwango cha juu.
Ushirikiano wa Messi, Neymar na Luis Suarez unastahili pongezi za
kipekee kwa kuwa hawakuwa wachoyo, ndiyo maana hata juzi wawili kati yao
walifunga huku mmoja akitengeneza mabao.
Fainali vs Juventus
Katika fainali ya juzi dhidi ya Juventus ambapo Barcelona ilishinda
3-1, usiku kipa chipukizi Marc-André ter Stegen, 23, hakuwa na kazi kubwa
lakini alionyesha kujiamini, anaonyesha dalili za kuwa kipa bora miaka ijayo,
hasa kama ataendelea kubaki klabuni hapo.
Mabeki wote walikuwa kwenye ubora wao, Dani Alves kama kawaida
alisaidia mashambulizi kwa kupanda, japokuwa mara kadhaa alijisahau na Juventus
kupata nafasi ya kupiga krosi kadhaa kutoka upande wake.
Gerard Pique ndiye beki aliyecheza vizuri kuliko wote, alipanda
kusaidia mashambulizi, aliokoa vizuri, alicheza mipira ya juu na aliwapanga
wenzake vizuri. Javier Mascherano alianza kwa kupaniki lakini baadaye alitulia
na kuonyesha ubora wake.
Jordi Alba kama ilivyo kwa Alves alipanda mara nyingi na kuchangia bao
la kwanza, hakuwa na kazi nzito ya kukaba.
Katika safu ya kiungo, ushirikiano wa Sergio Busquets na Ivan Rakitić ulikuwa na maana, wao ndiyo waliozima mashambulizi ya Juventus kutokea katikati.
Mkongwe Andrés Iniesta ndiye aliyekuwa injini ya Barcelona, kwa kuwa
vijana wake wawili nyuma walifanya kazi nzuri, hiyo ilimrahisishia kuuchezea
mpira, kuiendesha timu, kutoa pasi zenye macho na kuituliza Barcelona hasa
mwanzoni mwa kipindi cha pili ambapo walionekana kupoteana kiasi.
Messi inawezekana hakuonyesha yale makeke yake ya kuukokota mpira na
kuwapangua wapinzani lakini yeye na Iniesta ndiyo waliokuwa mafundi mitambo.
Messi alianza kutengeneza bao la kwanza kwa pasi yenye macho, kisha
akatengeneza la pili ambalo lilitokana na ule uwezo wake binafsi ambao
unajulikana.
Suarez licha ya kuwa staika wa kati lakini alifanya kazi nzuri ya
kuwasumbua mabeki wa Juventus, kuna muda alirejea katikati ya uwanja ili
kumsumbua Andrea Pirlo pindi Juventus walipokuwa wakimiliki mpira.
Kocha wa Barcelona, Luis Enrique alipanga kikosi kizuri na mbinu zake
zilifanikiwa. Mabadiliko aliyoyafanya yalikuwa na maana kubwa na faida, Jérémy
Mathieu aliingia kuzuia, Juventus wakapanda kujua wapinzani wao wamezidiwa,
wakajikuta wanapigwa la tatu kwa shambulizi la kushtukiza.
Xavi Hernandez aliingia kuituliza timu na akafanikiwa kwa hilo, Pedro
ni mjanjamjanja na ndiye aliyesaidia bao la tatu.
CHUKUA HIYO…
# Barcelona ni timu ya kwanza kutwaa mataji matatu makubwa katika
msimu mmoja mara mbili (2009 na 2015).
# Juventus imepoteza fainali za Ulaya mara sita, ni mara nyingi zaidi
ya timu nyingine yoyote.
# Wapinzani wote wa Barcelona msimu wa 2014-15 katika Ligi ya Mabingwa
walikuwa ni mabingwa wa nchi zao, PSG, APOEL, Ajax, Manchester City, PSG,
Bayern Munich, Juventus.
# Messi, Xavi, Iniesta na Pique wameifikia rekodi ya Calrence Seedorf
kutwaa taji la Ulaya mara nne tangu mwaka 1992.
# Fainali ya juzi ilikuwa mechi ya 99 kwa Messi katika Ligi ya
Mabingwa, amefunga mabao 77, ameasisti 22, jumla amechangia mabao 99.
# Beki wa Juventus, Patrice Evra alikuwa akicheza fainali yake ya tano
ya Ulaya, amefikia rekodi ya Seedorf na Edwin van Der Sar. Wote wanazidiwa na
Paolo Maldini.
# Iniesta ni mchezaji pekee wa Barcelona aliyecheza fainali nne za
Ulaya (2006, 2009, 2011 na 2015).
# Juventus ilikuwa na kikosi cha ‘wazee’ chenye wastani wa miaka 30.
0 COMMENTS:
Post a Comment