Na Saleh Ally
NIWAKUMBUSHE kwamba, tunapokwenda sasa ni pabaya, maana tunaanza
kuondoka katika afadhali na kutumbukia kunakoonekana ni mwisho kabisa wa shimo.
Najua utakuwa umesikia taarifa za mashabiki
kulishambulia gari la wachezaji wa Taifa Stars wakati wakiwa barabarani
wakienda mazoezini.
Walifanya hivyo mara ya kwanza hadi wakapasua kioo, jambo
ambalo kwangu nililiona ni la kusikitisha pale unaposikia wananchi wanaamua
kuwashambulia wanajeshi wao, tena wakiwa katika maandalizi ya kwenda kupambana
na adui ambaye hajulikani yuko katika ubora upi.
Nilijiliuza, wanaolishambulia basi hilo ni wananchi wa
aina gani ambao wanaweza kuonyesha mapenzi yao kwa kuwaumiza wadogo au kaka zao
ambao ndiyo wanaokwenda kupambana kwa ajili ya taifa lao?
Jibu haliwezi kupatikana kirahisi, wakati mwingine
unafikiria aliyefanya hivyo anaweza kuwa ni Mtanzania wa kuchovya, huenda
anatokea nchi jirani!
Kama ana hasira, basi angeweza kukaa kimya. Ikiwezekana
akasusa na kuacha kuishangilia timu kuliko kuishambulia. Mimi pia nachukizwa na
mwenendo wa Stars, lakini ndiyo timu ya nchi yangu. Kamwe kama mkono wako
ukinyewa, hauwezi kuukata. Inaendelea kubaki ni timu yangu ya taifa.
Juzi likatokea tukio jingine baada ya shabiki mwingine
kulishambulia basi la Stars likiwa katika makutano ya barabara za Uhuru na ile
ya kwenda gerezani. Basi likasimamishwa, wachezaji na baadhi ya watu wa benchi
la ufundi wakateremka na kuanza kumkimbiza mhusika, wakamkamata na kumtandika.
Kweli kupigwa kila wakati inaudhi, lakini najiuliza sasa
wachezaji nao wameanza kupiga mashabiki? Unaweza vipi kuwatofautisha na ule
ujinga wa shabiki aliyeshambulia basi la Stars?
Shabiki mpuuzi kashambulia na wachezaji nao wamefanya
upuuzi huohuo wa kushuka na kumshambulia shabiki! Sasa nani anasalimika katika
upuuzi huu?
Tumepiga hatua mbovu kabisa, kwamba sasa imekuwa ni vita
kati ya mashabiki wanaofanya upuuzi dhidi ya wachezaji wetu wa timu ya taifa
wanaofanya upuuzi zaidi, tena mbele ya viongozi wao walioshindwa kuwadhibiti.
Nidhamu ni mbovu?
Huenda mashabiki walikuwa na ujumbe wa kufikisha kwa
wachezaji kwamba pamoja na ubovu wa kocha Mholanzi, Mart Nooij, nao pia
hawajitumi au hawana msaada na timu na wanapaswa kubadilika.
Lakini walichukua njia ambayo si sahihi kwa
kulishambulia basi, jambo ambalo si sahihi kisheria, si vema kiungwana na si
tabia za Kitanzania. Kila mtu ana hasira, wakati mwingine vizuri kuzizuia.
Wachezaji kweli nao ni binadamu, wanaweza kukerwa na
tabia ya kushambuliwa, huenda wanaona hawana kosa na si haki wao kushambuliwa.
Sahihi kabisa, lakini tunabaki palepale kwamba bado wangeweza kumkamata mtu
huyo, halafu wakamkabidhi kwenye vyombo vya dola, si walivyofanya wao, tena
wakionekana ni watu muhimu katika kupigania na kulinda heshima ya nchi yetu.
Umeona tulipo sasa! Wachezaji wa timu ya taifa na
mashabiki wa timu ya taifa kuwindana mitaani, tena hata kabla ya mechi na
kuchapana.
Jambo baya kabisa katika picha ya soka ya Tanzania na
hii inaonekana kiasi gani sisi ni wajinga na tusiojitambua. Hatujui tuendako,
si watu tunaoweza kuheshimiana au kutumia njia sahihi za kufikishiana ujumbe au
kukatazana jambo.
Kizazi hiki kinaonekana kuwa na wazembe wengi ambao wazi
hawawezi kukisaidia kusonga mbele. Wachezaji wasio tayari kupambana vilivyo kwa
taifa lao, huenda kwa sababu posho imechelewa au kwa kuwa hawajiamini tu.
Mashabiki walio tayari kuishambulia timu yao ya taifa
ikiwa katika maandalizi ya mechi muhimu dhidi ya Uganda kuwania kucheza Chan.
Inawezekana ndiyo ujinga tuliozaliwa nao, lakini mwanadamu bora ni yule
anayebadilika.
Kweli Stars imepoteza, sasa mechi inayokuja kinachotakiwa
ni kuwapa moyo, si kuwashambulia kwa mawe. Tutumie njia sahihi kuwafikishia ujumbe.
Wachezaji nao, oneni aibu basi. Kila siku nyie tu, mambo
ya kubahatisha tu! Kama mnaona Mholanzi wenu uwezo wake ni mdogo, mshauri wa
ufundi wa Rais wa TFF naye ni mchanga na hana msaada wowote, basi tumieni uwezo
wenu binafsi na muisaidie timu. Kweli tunaumia na watu wanachoka. Aaah!
0 COMMENTS:
Post a Comment