YANGA ILIWAHI KUWEKA KAMBI NCHINI UTURUKI... |
Uongozi wa Klabu ya Yanga upo mbioni kutafuta kambi ya siku kadhaa
kati ya Afrika Kusini na Ureno kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu
pamoja na michuano ya kimataifa.
Yanga ambayo ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu
uliopita kwa mara ya 25, ipo katika mchakato wa kufanya usajili kabambe wa
kuhakikisha kikosi kinakuwa imara.
Aidha, imeelezwa kuwa timu hiyo itaanza kambi visiwani Zanzibar
kwa muda mfupi baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa
kuanza mwezi ujao.
Taarifa za ndani kutoka Yanga zimeeleza, wataanza na kambi ya
Zanzibar kwa siku kadhaa kwa ajili ya kujiandaa na Kagame kisha ikimalizika
michuano hiyo, wataamua kama kwenda Afrika Kusini au Ureno kwa kambi ya
kujiandaa na ligi kuu.
“Timu inaanza mazoezi Jumanne (jana) kwa ajili ya kujiandaa na
michuano ya Kombe la Kagame ambapo timu inatarajiwa kwenda Zanzibar kwa kambi
ya muda mfupi kisha itarejea Dar kwa ajili ya michuano.
“Baada ya hapo kocha Hans van Der Pluijm atachagua kambi kati ya
nchi mbili; Afrika Kusini na Ureno na uongozi utajadiliana na kuona timu iende
wapi kwani bado hatujaamua.
“Lengo ni kuhakikisha wanakuwa na kikosi bora kitakachokuwa na ushindani
msimu ujao kuanzia ndani hadi nje,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha kuzungumzia
suala hilo, alisema: “Kwa sasa bado hatujapanga mipango yoyote juu ya suala
hilo, maamuzi mengine yatakuja baadaye.”
0 COMMENTS:
Post a Comment