Kocha, Piet De Mol raia wa Ubelgiji, ameendelea
kuonyesha nia ya kutua kwenye klabu ya wakata miwa, Mtibwa Sugar, baada ya
viongozi wa timu hiyo kuthibitisha kuwa juzi Jumatatu alitembelea klabuni hapo.
Licha ya kutofanya mazungumzo yoyote ya kumpa mkataba, lakini
uongozi huo umesema kuwa kocha huyo alifika Manungu, Turiani kwa ajili ya
kuangalia mandhari pamoja na kambi ya wachezaji kwa ujumla na namna
wanavyoishi.
Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alithibitisha ujio wa
kocha huyo klabuni hapo ambapo alidai kuwa licha ya kuwatembelea lakini bado
hawajafanya mazungumzo yoyote kuhusu usajili japokuwa nia ya kuzungumza naye
ipo.
“Ni kweli jana (juzi) Jumatatu De Mol alifika hapa klabuni kwa
ajili ya kucheki mandhari pamoja na kambi ya wachezaji wetu kwa ujumla.
“Licha ya kutua hapa, hatuna maana ya kwamba tumeshamsajili,
hapana, tunaomba tu mashabiki wetu wawe na subira, pindi tutakapomalizana naye
tutawajuza kinachoendelea kwani nia tunayo juu yake,” alisema Kifaru.
0 COMMENTS:
Post a Comment