Kikosi cha Azam FC, juzi Jumamosi ilifanikiwa kuweka rekodi kwenye
michuano ya Kombe la Kagame baada ya kumaliza hatua ya makundi bila ya kuruhusu
wavu wake kutikiswa.
Azam iliyokuwa Kundi C, imeweka rekodi hiyo baada ya kuanza
michuano hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KCCA ya Uganda na kufuatiwa na
ushindi wa 2-0 mbele ya Malakia ya Sudan Kusini na kuhitikisha kwa kutoa kipigo
kitakatifu cha mabao 5-0 kwa Adama City ya Ethiopia.
Wanalambalamba hao, wamemaliza hatua hiyo ya makundi wakiwa vinara
kwenye kundi lao, kufuatia kujikusanyia pointi tisa, wakifuatiwa na KCCA wenye
pointi sita.
Wakati Azam ikiweka rekodi hiyo, nayo Telecom ya Djibouti, kabla
ya mchezo wa jana dhidi ya Gor Mahia ya Kenya ilikuwa ni timu pekee ambayo
ilikuwa haijafunga bao lolote, ikifuatiwa na Adama City ambayo imeliona lango
mara moja tu.
Kutokana na Azam kuonekana kuwa na ukuta mgumu mpaka sasa, kocha
wa kikosi hicho, Muingereza, Stewart Hall, aliliambia Championi Jumatatu kuwa,
mfumo wa 3-5-2 anaoutumia kwenye michuano hiyo ndiyo unampa matokeo hayo.
“Niliujaribu mfumo huu mara ya kwanza tulipocheza dhidi ya KCCA na
wachezaji wangu walionekana kucheza kwa kuelewana sana na hatimaye nyavu zetu
hazikuguswa, nitaendelea kuutumia tena na tena hata kwenye ligi kuu,” alisema
Hall.
0 COMMENTS:
Post a Comment