JUMA ABDUL (KUSHOTO) AKIWA NA MZEE AKILIMALI... |
Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amesema kuwa
kuumia kwa beki wake wa pembeni, Juma Abdul, ndiyo kumesababisha wao waondolewe
kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mechi ya robo
fainali dhidi ya Azam FC, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam na Yanga kufungwa kwa penalti 5-3.
Juma alitolewa nje baada ya kugongwa kifuani na mshambuliaji wa
Azam, Ame Ally, katika dakika ya 75 na kusababisha apoteze fahamu kabla ya
Pluijm kufanya mabadiliko kwa kmuingiza, Joseph Zuttah.
Pluijm alisema kutoka kwa beki huyo kuliharibu mipango yake yote
ya ushindi kwenye mechi hiyo iliyojaa upinzani.
Aliongeza kuwa, pia safu yake ya ushambuliaji ilichangia kwa kiasi
kikubwa wao kutolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Kagame, kutokana na
kushindwa kutumia nafasi nyingi.
Safu hiyo ya ushambuliaji ya Yanga iliongozwa na Mzimbabwe, Donald
Ngoma, Amissi Tambwe, Geofrey Mwashiuya, Deus Kaseke kabla ya kutolewa na
nafasi yake kuchukuliwa na Malimi Busungu.
“Nikiri kuwa, kuumia kwa Juma kwenye mechi hii dhidi ya Azam na
kusababisha ashindwe kuendelea na mechi hii kumechangia kwa kiasi kikubwa
tuondolewe katika michuano ya Kagame.
“Ninaamini kuwa, kama asingeumia Juma katika mechi hii, basi
matokeo yasingemalizika hivi, kufungwa kwa penalti.
“Pia, washambuliaji wangu walichangia nao tupoteze mechi hii
kutokana na kushindwa kuzitumia nafasi nyingi walizokuwa wanazipata uwanjani.
“Nawapongeza viungo wangu, kiukweli walitengeneza nafasi nyingi za
kufunga mabao, lakini washambuliaji Ngoma na Tambwe walishindwa kuzitumia,” alisema
Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment