Kufuatia
presha ya shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS), mshiriki mwenye
namba 08126 ambaye jina lake halikuweza kupatikana, alijikuta katika wakati
mgumu kutokana na kupoteza fahamu baada ya majaji kumwambia hana nafasi ya
kuendelea kushiriki.
Usaili wa
BSS kwa Dar es Salaam ulianza juzi na unatarajiwa kufikia tamati leo Ijumaa
ambapo zaidi ya washiriki 1,000 wamejitokeza katika kinyang’anyiro hicho ambapo
watakaopatikana wataunganishwa na washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Arusha na
Mbeya.
Mshiriki
aliyekutwa na majanga hayo alianguka na kuzimia baada ya Jaji Joachim Kimario
‘Master Jay’ kumtaka aondoke jukwaani kutokana na kutoimba vizuri, hali ambayo
ilisababisha akimbizwe hospitali.
Mkurugenzi
wa Benchmark Production, Rita Poulsen ‘Madam Rita’, amesema tukio hilo
limetokea bahati mbaya na kudai kuwa wana kibarua kigumu katika kuwapata
waimbaji kwa kuwa wengi waliojitokeza ni wenye vipaji vya kawaida tofauti na
mikoa mingine.
“Bado
tunaendelea na usaili washiriki waliojitokeza ni wengi mno kwa upande wa Dar,
lakini tuna wakati mgumu kwani tumeshapitia washiriki wengi lakini hatujapata
wale wa kutusisimua, labda hadi tutakapomaliza.
“Mara
baada ya kuwapata tutawachuja washiriki mpaka wabaki 50, kisha tutakuwa na ‘top
20’ kisha ‘top 5’ kisha kusaka mshindi,” alisema Madam.
0 COMMENTS:
Post a Comment