Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Godfrey Mwashiuya kweli anatisha, wakati
Wabongo wakimsifia kuwa anaweza kuwa staa wa baadaye wa timu hiyo, hilo
limeonekana kuwa njiani kutimia, ndiyo maana mabeki wa timu ya Télécom ya
Djibouti waliamua kutumia nguvu ya ziada kumzuia.
Mwashiuya ambaye alifunga bao moja katika mechi dhidi ya wapinzani hao
katika Kombe la Kagame, juzi Jumatano, alijikuta akiwa katika wakati mgumu
kutokana na mabeki wa Telecom kumchezea kibabe muda mwingi wa mchezo huo ambao
alifunga bao kali.
Katika mchezo huo ambao Mwashiuya aliingia kipindi cha pili kuchukua
nafasi ya Simon Msuva, alikabwa kibabe na nahodha wa Telecom, Mohamed Wais Ali
kiasi cha kumsababishia maumivu makali shingoni ambayo yangeweza kusababisha
apoteze maisha kwa kushindwa kupumua.
Picha hapo juu ilibaini ubabe huo aliokuwa akichezewa Mwashiuya hata
kama hakuwa na mpira dhidi ya nahodha huyo ambaye alionekana wazi kufanya hivyo
ili kumtoa mchezoni Mwashiuya.
Yawezekana kutokana na ugeni wa mechi ngumu au za kimataifa, licha ya
kubanwa kibabe na kuchezewa rafu mara kadhaa bado Mwashiuya alishindwa
kuonyesha kujibu mapigo mbele ya beki huyo zaidi ya yeye kumtesa kila alipokuwa
akipata mpira.
Kamera yetu ilimnasa Mwashiuya akikabwa koo kwa nguvu na Wais Ali
ambaye wazi hakuonekana kuwa na huruma hata kidogo.
Wais Ali alitumia nguvu kubwa kumbana kooni kiungo huyo kiasi cha
kusababisha akose pumzi na kuanguka chini lakini mwamuzi hakutoa kadi yoyote.
Alipoulizwa juu ya suala hilo na mchezo huo kwa jumla, Mwashiuya
alisema: “Nimekatazwa kuzungumza lolote na vyombo vya habari.”
Daktari wa Yanga, Juma Sufian akizungumzia kuhusu kilichotokea kwa
Mwashiuya alisema:
“Alipatwa na maumivu ya koo baada ya kukabwa, tulilazimika tumpe
huduma ya kwanza mara tatu hivi, ilikuwa ni kumtuliza maumivu aliyokuwa nayo,
baada ya mechi tulimuangalia alikuwa na alama za kucha kidogo chini ya kidevu
na uvimbe kwenye sehemu za koo.
“Unajua aliumia na kupata maumivu makali kwa sababu kuna wakati
alikabwa mpaka akavutwa koromeo, ndiyo maana ana maumivu mpaka leo asubuhi
(jana), hata mazoezini alikuwa na uvimbe kidogo.”
Kuhusu madhara ya tukio hilo, anafafanua: “Kama angemuumiza zaidi
athari zake ni kwamba angeweza kuvimba kwenye koo ndani au nje na inaweza
kusababisha kushindwa kumeza na kupata maumivu zaidi ya hapo. Ikifikia hatua
hiyo basi angeweza kuugua zaidi.”
SOURCE: GAZETI LA CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment