Saleh Ally na
Mtandao
UVUMILIVU wa
makocha wakati mwingine umekuwa ukilipa, mfano mzuri ni pale Arsene Wenger
alipoonyesha uvumilifu mkubwa wakati Robin van Persie akiwa ‘kimeo’.
Karibu misimu
miwili, van Persie alikuwa ‘tiamaji tiamaji’, Wenger akamvumilia hadi
aliporejea kikosini na kuwa msaada mkubwa.
Mwisho, van
Persie aliipatia Arsenal faida baada ya kuuzwa kwa kitita cha pauni milioni
22.5, safi kabisa.
Safari hii ni
zamu ya Theo Walcott, mchezaji ambaye amekuwa akijulikana kama kinda. Ingawa
kwa sasa ameshaondoka huko, maana ana umri wa miaka 26, kisoka huyu tayari ni
mchezaji aliyepevuka.
Msimu ujao wa
2015-16 utakuwa ndiyo wa uamuzi hasa kwa Walcott na dalili zote zinaonyesha
kuwa ndiye atakuwa shujaa wa Arsenal kwa mambo mengi tu yakiwemo kitakwimu,
kwani tayari ameshaanza kuonekana tishio kwenye mechi za maandalizi, utakumbuka
juzi alifunga bao wakati Arsenal ikiichapa Everton 3-1.
Uzoefu:
Ingawa alikuwa
nje ya uwanja kwa muda mrefu, Walcott mwenye asili ya Jamaica, anabaki kuwa
ndiye fowadi mwenye uzoefu zaidi na soka la England katika kikosi hicho cha
Wenger.
Hauwezi
kumlinganisha na Mesut Ozil, Olivier Giroud au Alexis Sanchez, hivyo ndiye
anayeweza kuwa kiongozi wa jahazi la utengenezaji na upachikaji mabao.
Ameonyesha
kuwa atakuwa tegemeo, kwani baada ya kurejea msimu uliopita, ingawa alikuwa
akipata nafasi chache za kucheza, lakini alifunga mabao na kutengeneza kadhaa.
Kwa
kushirikiana na wakali ambao Arsenal imejaza katika safu yake ya ushambuliaji,
Walcott anaweza kuwa msaada zaidi na kiongozi wa kufunga.
Tayari
amefunga mabao 50 ya Ligi Kuu England akiwa na Arsenal aliyojiunga nayo mwaka
2005 akitokea Southampton aliyoichezea msimu mmoja katika Ligi Daraja la Kwanza
England.
Kufunga
hakiwezi kuwa kitu kigumu kwake, wala hawezi kuwa na hofu na beki wa aina
yoyote.
Uchezaji:
Tayari Wenger
amelizungumzia hilo, kwamba uchezaji wa Walcott unaonyesha kuwa ni mchezaji
aliyepevuka.
Miaka mitano
iliyopita, Walcott alitaka kuzichapa uwanjani na van Persie aliyemtuhumu kuwa
na tabia za ‘kitoto’ kung’ang’ania mpira bila sababu za msingi. Kweli moja ya
matatizo ya wachezaji makinda ni “anao anao”.
Kwa sasa
inaonekana kuwa ana uchezaji tofauti, zaidi anachoangalia ni faida kwa timu na
kwa kuwa ameichezea Arsenal mechi 208 za Premier League, inatosha kuthibitisha
kwamba ni mchezaji anayefanya anachokijua.
Miaka 10:
Tayari
amekamilisha misimu 10 ya Premier League. Si haba, tena anakuwa mchezaji
anayeongoza kwa kuitumikia Arsenal kwa miaka mingi katika safu ya ushambuliaji.
Uzoefu huo
unampa urahisi wa kufanya vizuri zaidi. Lazima ukumbuke Arsenal inashiriki
michuano ya aina tatu England ambayo ni Premier League, Kombe la FA na Kombe la
Ligi na yote Walcott amecheza.
Sasa ndiyo wakati
mwafaka wa yeye kuonyesha kweli anapaswa kuwa msaada na ana uwezo wa kusaidia
Arsenal iwapo atashindwa msimu huu, huenda ikawa ameshindwa kabisa.
Jezi namba 14:
Wakati
anakabidhiwa jezi namba 14, kwake ilikuwa mzigo mkubwa. Unakumbuka kabla ya
yeye kuichukua, ilikuwa mali ya nani?
Si unamkumbuka
Thierry Henry? Gwiji, jamaa hatari aliyekuwa anajua afanye nini na mpira kwa
ajili ya matokeo bora katika kikosi chake.
Wakati Walcott
alipokabidhiwa, alieleza namna ambavyo alifurahia kuivaa jezi hiyo, lakini deni
lilikuwa likimtafuna.
Huenda huu
ndiyo wakati mzuri kwake kulipa na msimu ujao unapaswa kuwa majibu. Kama
atashindwa kuwa kiongozi au nyota wa mashambulizi ya Arsenal, dalili
zinaonyesha atakuwa anajisogeza mlangoni.
Kama Arsenal
itashindwa kuona inamtegemea Walcott msimu ujao, maana yake utakuwa ni mwaka wa
11 ikiwa naye. Hivyo itakuwa ni kipindi mwafaka cha kuangalia haya mawili;
kumuuza au kumuacha azeekee Emirates.
Maana yake
Arsenal wanaweza kuwa na mawili, kumuangalia msimu ujao kwamba ameonyesha yeye
ni tegemeo na ana msaada mkubwa, basi abaki.
Ikionekana
pamoja na uvumilivu wa Wenger, bado ni tiamaji tiamaji, basi ili kuepusha miaka
30 kumkuta akiwa hapo, watampiga bei.
Huu ndiyo
wakati mwafaka kwa Walcott kuamua mwenyewe. Msimu wa 2015-16 utakuwa fainali
kwake ambayo itakuwa inaamua kumbakiza au kumuondoa Arsenal aliyoitumikia kwa
miaka 10 katika Premier League.
Mabao yake 50
ya Premier League, bado hayampi nafasi ya kuwa gwiji wa Arsenal kwani kwa
misimu 10 ukiyagawanya utapata 5 kila msimu.
Walcott
hajafanikiwa kubeba ubingwa wa Premier League akiwa na Arsenal. Amebeba Kombe
la FA na Kombe la Ligi.
Huu ndiyo
wakati wa kuisaidia Arsenal kutimiza kiu yake hiyo kwani haijabeba kombe hilo
tangu mwaka 2004, pia inataka kufika mbali zaidi katika michuano ya kimataifa.
Kikosi chake
ni bora, Walcott anacheza katikati ya mafundi wenzake. Bila shaka hawezi
kulalamika kukosa msaada. Kwa watu anaocheza nao, halafu akashindwa kufanya
vema dalili za safari zitakuwa wazi maana Arsenal nayo kama timu makini itaanza
kuhofia ‘uzee’ wake au ‘ukimeo’ wake kwa kuwa ni timu yenye filosofia ya ujana.
Kama ni
kutengeneza rekodi nzuri yenye majibu ni sasa, yaani msimu ujao. Kwani tayari
ni mzoefu, mwenyeji na yuko fiti na kwa mwonekano wa msimu uliopita baada ya
kurejea, inaonekana hivi; asipoumia, hakika hakuna atakayemzuia kuwa tishio,
ila akishindwa, safari itamkuta.










0 COMMENTS:
Post a Comment