Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma,
amejutia mno kadi yake nyekundu aliyopewa kwenye mechi dhidi ya Gor Mahia ya
Kenya na akakiri kuwa, yeye ndiyo chanzo cha Yanga kufungwa lakini upande wa
pili hali imekuwa tete baada ya makocha kumponda kwa alichokifanya.
Ngoma alizawadiwa kadi ya pili ya njano kabla ya kuonyeshwa nyekundu
na kwenda nje kwenye dakika ya 23 baada ya kumsukuma Haruna Shakava wa Gor.
Kabla ya hapo, Ngoma alikuwa mwiba kwa safu ya mabeki wa Gor kutokana na
usumbufu aliokuwa nao na kusababisha bao la kuongoza kwa timu hiyo mapema
dakika ya nne.
Hata hivyo, baada ya hapo Yanga ilionyesha wazi kuwa na upungufu
uwanjani na mwisho wa siku, Gor wakaibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo
huo wa kwanza wa Kombe la Kagame uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Kuhusiana na hilo, mara baada ya mechi hiyo kwisha Ngoma alikiri
kuidhoofisha Yanga baada ya yeye kutoka lakini akapiga moyo konde na kusema
kuwa ana imani watafanya vizuri kwenye mechi zijazo na watasonga mbele kwa
kishindo.
“Wanisamehe sana, sikupenda iwe hivi lakini imetokea, sijisikii
vizuri kwa kuwa nimekuwa sababu ya Yanga kufanya vibaya kwenye mechi ya kwanza,
upungufu wa wachezaji uwanjani kwa timu kama Gor ilikuwa ni kigezo cha kwanza
kuzidiwa.
“Nimeona wachezaji wenzangu walivyopambana lakini imeshindikana,
ila naiamini sana timu yangu, ingawa tumepata matokeo mabaya ya kwanza, bado
tuna mechi mkononi na najua tutafanya vizuri, tutasonga mbele.”
Kocha wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm naye aliikosoa kadi
hiyo kwa kusema wazi kwamba kwa mchezaji profesheno kama Ngoma hakusatahili
kufanya makosa kama yale lakini kwa kuwa imeshatokea hana la kufanya.
“Kilichotokea hakikuwa sawa kulingana na maamuzi aliyoyachukua
Ngoma, yeye kama mchezaji profesheno alipaswa kutambua kwamba tayari ana makosa
na ana kadi moja hivyo ilimpasa kujilinda lakini akalisahau hilo na mwisho yakatokea
yaliyotokea,” alisema Pluijm.
Kocha wa Simba, Mwingereza, Dylan Kerr, aliyekuwepo uwanjani hapo,
naye alizungumza juu ya hilo: “Alichokifanya si kitendo cha kiuchezaji, amekuwa
na hasira akashindwa kujizuia na akaigharimu timu na hasara ni kwa Yanga sasa,
mchezaji hutakiwi kuwa hivyo halafu ukizingatia ni mtu muhimu, anapaswa kufuata
falsafa za michezo uwanjani na kuisaidia timu yake na si vingine.”
Ngoma atakuwa nje ya uwanja kwenye mechi inayofuata dhidi ya Telecom
ya Djibouti itakayopigwa keshokutwa Jumatano, kisha kurejea kwenye mechi dhidi
ya KMKM ya Zanzibar.







Yanga walijaribu sana kwa kuonyesha mchezo mzuri licha ya kuwa na kadi nyekundu.
ReplyDelete