Na Saleh Ally
ALIYEKUWA
mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi inawezekana ndiye mchezaji mwenye akili
kuliko wengine wote waliowahi kucheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara tangu
kuanzishwa kwake.
Utakapozungumzia
mafanikio, basi Nonda Shabani ‘Papii’ anaweza kuwa ndiye mwenye mafanikio zaidi
baada ya kupata nafasi ya kucheza Afrika Kusini, Italia, Ufaransa na England.
Unapozungumzia
suala la biashara, basi haliwezi kupita bila ya kuwataja Wachaga. Okwi anabaki
kuwa mchezaji mwenye akili zaidi ya biashara kwani ndani ya miaka saba
aliyocheza Tanzania, amefanya biashara iliyotengeneza zaidi ya Sh bilioni 1.7.
Fedha hizo,
hakuna mchezaji yeyote wa Tanzania au mgeni ukiachana na Nonda ambaye amewahi
kuifanya isipokuwa Okwi ambaye amecheza zaidi ya timu nne katika nchi nne.
Alitua
Tanzania mwaka 2008 akitokea SC Villa, binafsi ameweza kutengeneza zaidi ya Sh
milioni 500 kama sehemu ya uhamisho tu, lakini ukijumlisha malipo yake yote
anakuwa ni mchezaji ghali zaidi kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Lakini
utagundua kuwa Okwi si mchezaji mwenye kipaji cha uwanjani tu, badala yake ni
mchezaji anayejua kwa nini anacheza mpira na anataka nini ndani na nje ya
uwanja, ndiyo maana ameweza kuchota fedha nyingi kuliko wachezaji wote walio
katika Ligi Kuu Bara.
Huenda unaweza
kufikiri Mbwana Samatta anayelipwa mshahara wa dola 10,000 (Sh milioni 20)
anaweza kuwa na fedha nyingi kuliko Okwi. Hapana! Mganda huyo, ameweza kuingiza
fedha nyingi haraka katika masuala ya uhamisho.
Karibu kila
uhamisho alioufanya, Okwi anaonekana aliutengeneza kutokana na mahitaji ya timu
husika. Ingawa kikubwa namba moja imekuwa ni ngao yake ya juhudi na utendaji
bora kabisa anapokuwa uwanjani. Baada ya hapo timu humhitaji, naye hafanyi
ajizi.
Wakati anatoka
SC Villa kujiunga na Simba, Waganda hao walilipwa Sh milioni 20, huku Okwi
akipata Sh milioni 5. Simba ilimuuliza Etoile du Sahel kwa dola 300 (Wakati huo
zikiwa ni Sh mil 480).
Wakati Simba
haikupata kitu, Okwi alilamba dola 100,000 (Sh milioni 160 wakati huo)
kulingana na makubaliano. Simba ikaambulia patupu.
Baadaye Yanga
ikatoa Sh milioni 160 kumsajili Okwi ikidai imemtoa SC Villa ingawa hali halisi
alikuwa mchezaji wa Etoile. Okwi alilamba Sh milioni 100 ingawa hakumaliziwa na
Yanga na mgogoro ndipo ulipoanzia hadi akatimkia Simba ambao walimpa mshahara
mzuri wa dola 3,500 lakini hawakumlipa fedha za usajili.
Baada ya muda
mchache walimpa miezi sita kufanya awe na mkataba wa mwaka mmoja, wakamlipa
dola 20,000 (zaidi ya milioni 36 wakati huo). Simba wakaona itakuwa vizuri
kumuongezea mwaka mzima tena, hilo likafanyika nao wakatoa dola 40,000 (zaidi
ya Sh milioni 72) ingawa hadi anaondoka hakuwa amemaliziwa dola 5,000.
Simba imemuuza
Sonderjyske kwa dola 110,000 (zaidi ya Sh milioni 220), naye amedaka chake. Hii
inamfanya awe ameingiza zaidi ya Sh milioni 500 kwa upande wake.
Upande wa
biashara kwa maana ya timu, biashara ya zaidi ya Sh bilioni 1.5 timu kwa timu
imefanyika ingawa kuna fedha hazikulipwa kama zile alizotokea Simba kwenda
Etoile.
Okwi ni
mchezaji anayejua anafanya nini na huu ni mfano ambao unauona amegundua mambo
mawili makuu katika maisha yake ya soka. Kutokana na kujiamini amekuwa
akiyafanya.
Kwanza,
Tanzania ni “Shamba la Bibi” hivyo ni rahisi kwake kuendelea kuchuma, wachezaji
wa Kitanzania na viongozi wa Kitanzania wapo tu. Kwa wachezaji hakuna mwenye
juhudi ya kufanya kazi ili apambane hapa nyumbani au nje naye aingize mamilioni
kama ya Okwi.
Pili amegundua
katika soka kuna fedha, pamoja na matatizo yake amekuwa akijituma kwa kila
namna kuhakikisha anakuwa tegemeo katika timu, nyota kila anapokwenda.
Usishangae ukaambiwa ametoka Denmark kurejea Tanzania, safari hii akiwa Azam FC
ambao wanaweza kuwa tayari kutoka Sh milioni 300 kumsajili!







0 COMMENTS:
Post a Comment