Baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano na klabu yake mpya ya Sonderjyske
ya nchini Denmark, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi,
amefunguka kuwa anaishukuru klabu yake hiyo ya zamani.
Okwi amewatumia Simba waraka wa kuwashukuru lakini pia akimshukuru
kocha wake wa sasa, Jakob Michelsen, ambaye alimfuatiliwa kwenye michezo 20
kabla hajampa nafasi.
Okwi amefanikiwa kuuzwa nchini humo mapema mwezi huu mara baada ya
kufuzu vipimo vya afya.
Okwi amefunguka hayo kupitia ukurasa wa Mtandao wa Twitter kwa
kuwashukuru mashabiki wa Simba na Waganda kwa kuweza kumsapoti na kufanikiwa
kucheza soka la kulipwa Ulaya.
“Napenda kuwaambia rasmi kuwa nimejiunga na Klabu ya Sonderjyske
kwa muda wa miaka mitano na napenda kumshukuru kocha, Jakob Michelsen ambaye
alikuwa akinifuatilia kwenye michezo 20 na kuweza kuvutiwa na uwezo wangu.
“Shukrani zangu za dhati ziende kwa Klabu ya Simba kwa mchango wao
mkubwa kwangu na kuweza kufika hapa nilipo sasa bila kuwasahau mashabiki wangu
wa timu ya taifa ya Uganda na mashabiki wangu wote kwa jumla. Ninapata meseji
zenu na simu, lakini nashindwa kuwajibu wote, tambueni niko pamoja nanyi na
nawapenda.
“Nitapambana huku Ulaya kuhakikisha naweza kuinufaisha klabu yangu
japo nafahamu wazi na kupambana na changamoto mpya,” aliandika Okwi.
Michelsen aliwahi kuwa kocha wa vijana wa timu ya taifa pamoja na
kocha msaidizi wa Taifa Stars.







0 COMMENTS:
Post a Comment