Wakati Simba ikiwa kwenye mchakato wa kupata
mshambuliaji kutoka Brazil, mchakato huo umepata kikwazo baada ya mwakilishi wa
klabu hiyo aliyetakiwa kwenda Brazil kusitisha zoezi hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba,
Zacharia Hans Poppe ambaye ndiye aliyetakiwa kusafiri kumfuata mchezaji huyo,
amesitisha mchakato wa usajili kutokana na uchaguzi wa urais ambao unatarajiwa
kufanyika baadaye mwaka huu.
Hans Poppe ambaye alikuwa asafiri jana Alhamisi,
amesema amelazimika kuahirisha safari hiyo kwa kusubiria kujiandikisha kupiga
kura ili kupata kitambulisho ambacho kitamwezesha kupiga kura ya kumpata rais
wa nchi kuchukua nafasi ya Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake wa kuwa
madarakani mwaka huu.
“Nilikuwa niondoke leo (jana), lakini nahitaji
kupata kitambulisho hicho. Awamu ya kwanza sikujiandikisha, kwa hiyo nimeona
iwapo nitaondoka, nitakosa tena kujiandikisha na sitapiga kura. Kwa vyovyote
vile safari itakuwa baada ya mchakato huo,” alisema kiongozi huyo.
Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 25,
mwaka huu, kuchagua rais, wabunge na madiwani lakini uandikishaji wa
vitambulisho unatarajiwa kuanza Julai 16 jijini Dar.
Hans Poppe aliongea kwa kusema: “Tayari kila kitu
kimekamilika kuhusu Mbrazili huyo na kilichobaki ni kwenda tu kumalizana naye
kulekule na kurejea naye.”
0 COMMENTS:
Post a Comment