Simba wamezinduka! Katika kile kinachoonekana Simba imepata
uongozi makini, timu hiyo imeshtuka kutoka mikono kapa katika mauzo ya kiungo
mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi, aliyejiunga na Klabu ya Sonderjyske ya
Dernmark na kuweka ngumu kuachia ITC yake ili kuwa mchezaji halali wa klabu
hiyo.
Bado Simba wanakumbuka machungu ya kunyimwa kitita cha dola
300,000 kwa mauzo ya nyota huyo mwaka 2012, katika Klabu ya Etoile du Sahel ya
Tunisia, wakati wa utawala wa Ismail Aden Rage, ambazo zimekuwa zikipigwa
danadana hadi leo hii.
Hata hivyo, katika kuhakikisha hawarudii makosa, utawala mpya
chini ya rais Evans Aveva, ulimuachia nyota huyo kwa masharti magumu na
mojawapo ni kwamba ITC yake itatoka pindi watakapoleta malipo ya mchezaji huyo.
Habari zinaeleza kuwa, Simba watakunja kitita cha dola laki moja
na kumi (110,000) ambazo ni zaidi ya Sh mil 200 kwa ajili ya mauzo ya staa huyo
raia wa Uganda.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, Said Tully, alisema
tayari makubaliano kuhusu malipo yamekamilika na wanatarajia kuingiziwa mkwanja
wao ndani ya wiki hii.
“Kuna mchakato mrefu kidogo katika ulipaji, lakini tunashukuru
kuwa tumekubaliana kwa kila kitu na ndani ya wiki hii tutapewa chetu. Hatuna
shaka na malipo na bahati mbaya au nzuri, bado ITC yake haijatoka, maana ndiyo
yalikuwa makubaliano ya pande mbili, kwamba ITC itatoka tu baada ya kukamilisha
malipo ya kumuuza,” alisema Tully.
Aidha, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kusema kuwa
hawana sababu ya kuumiza vichwa kuwaza nani mwenye kuziba pengo lake, kwa kuwa
ndani ya timu hiyo kuna wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu.
“Wapo wachezaji wenye uwezo wa kucheza nafasi yake, lakini pia ni
changamoto kwa vijana wengine ambao watakuwa na ari ya kutaka kuwa kama Okwi
ili waonekane na kupata maisha mazuri,” aliongeza Tully.








Kweli haya mambo ya ajabu,miaka minne nyuma Okwi aliuzwa kwa dola 300,000;leo Okwi anauzwa kwa dola 110,000!?
ReplyDeleteHapa ni usanii wa viongozi wetu kutaka kujirudishia pesa zao za usajili tuu.Kiwango cha Okwi hiwezekani akauzwa kwa chini ya dola 300,000 kwasasa.Viongozi acheni ujanja wenu kama mliotumia kwa Singano!