Na
Saleh Ally
LIGI
Kuu Bara inatarajiwa kuanza Agosti 22, mwaka huu, safari hii ikiwa na timu 16.
Hadi sasa bado ratiba haijatoka na imeelezwa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ndiyo
wanaifanyia kazi!
Ratiba
ya ligi kuu imekuwa sehemu kubwa ya matatizo yanayoyumbisha soka nchini, huenda
kwa kuwa umakini umekuwa si asilimia kubwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
imeshindwa kulithibitisha hilo.
TPLB
inapaswa kujua ratiba inapokuwa na viraka rundo au figisufigisu, basi inaleta
madhara rundo, pia inachangia kupunguza utamu wa ushindani na ladha ya wengi
kutaka kushuhudia mechi za ligi. Kwa kuwa Bodi ya Ligi bado haijatoa ratiba
hiyo, mambo haya matano kama yatafuatiliwa, basi yanaweza kusaidia kuwa na
ratiba bora ambayo itazaa ligi bora.
Mapema:
Miezi
miwili kabla ya ligi kuanza, klabu za Ligi Kuu England zimeshajua ratiba,
zitacheza na nani na kipindi kipi.
Kwa
Tanzania hilo limekuwa tatizo, lakini utaona timu zinazoshiriki tayari
zimejulikana, viwanja vinajulikana. Hivyo hakuna sababu ya kuendelea na
utaratibu huo wa zamani. Inapaswa kuanzia wiki ijayo ratiba iwe imetoka na timu
zijipange mapema kabla ya kuanza safari za ligi hiyo.
Wakati
mwingine, inakuwa rahisi timu kupata hata wadhamini wa kusaidia safari zao kwa
kuwa tayari mapema zinajua tarehe ipi zitakwenda wapi.
Biashara:
Hakuna
ujanja, wahusika lazima wakubali yote yanafanyika lakini ili kuzimudu gharama
za uendeshaji wa timu na klabu kwa jumla lazima faida ipatikane.
Inawezekana
udogo wa timu ukachangia timu kutoingiza faida kubwa lakini upangwaji wa ratiba
ukiwa wa kitaalamu, una nafasi ya kupunguza gharama kwa timu husika.
Mfano
timu inayotoka Mbeya kwenda Tanga, inapofika ni vizuri ikacheza mechi mbili kwa
kuwa pale kuna timu tatu. Inawezekana pia isiwe vizuri kuipa nafasi ya kucheza
mechi tatu pale Tanga, nayo itakuwa si nzuri kwa kuwa itaondoa hamu ya
mashabiki kuiona timu hiyo mara tatu mfululizo.
Angalau
mechi mbili, mechi nyingine itarejea mzunguko ujao. Kikubwa ni kuziweka timu
katika mazingira mazuri ambayo yatasaidia upunguzaji wa gharama angalau
zijimudu kwenye uendeshaji kwa asilimia mia, ikiwezekana zipate hata faida
kidogo.
Mechi
2 wilaya moja:
Mara
kadhaa katika mizunguko miwili iliyopita, zimekuwa zikichezwa mechi mbili siku
moja. Tena zinachezwa katika wilaya moja ya Temeke, umbali wa kilomita chache
kutoka uwanja mmoja kwenda mwingine.
Yanga
inacheza na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Taifa, halafu Stand inacheza na Ruvu JKT
pale Azam Complex. Hii ni kuziua kabisa hizi timu nyingine. Kuna uwezekano wa
ratiba ikapangwa vizuri, nazo zikapata mashabiki zaidi, maana bado hazijawa na
nguvu kama ile ya Simba au Mtibwa Sugar. Pia vizuri kukumbuka Stand wamesafiri
kutoka Shinyanga na wanahitaji fedha za geti kama kikuza mapato.
Muda:
Kuwa
na timu 16 kusiifanye ligi ichezwe mechi nyingi zaidi katikati ya wiki. Mara
nyingi watu wanashindwa kujitokeza katika mechi zinazochezwa katika kipindi
hicho.
TPLB
na TFF lazima wajue soka sasa ni biashara, hivyo ziangalie timu ambazo
zinapaswa kucheza wikiendi kwa kuwa zitavuta watu wengi iwe uwanjani hata
kwenye runinga.
Kupeleka
mambo harakaharaka yaishe tu haitakuwa sawasawa. Maslahi ni sehemu ya
kutengeneza ligi bora kwa kuwa timu zinapopata fedha nyingi, zinakuwa imara na
kuongeza ushindani.
Kuahirishwa:
Huu
ni ugonjwa mkubwa sana, TPLB na TFF kama wanataka mapinduzi, huu ndiyo wakati
mwafaka wa kuhakikisha wanaanza kupambana na jambo hili, kuahirishwa kwa mechi
za ligi bila sababu zisizokuwa na msingi hata kidogo.
Tabia
ya kuahirisha mechi hovyo inazua hisia rundo na nyingine zinakuwa na mwelekeo wa
ukweli, kwamba kuna timu inajengewa mazingira mazuri ili iwe na nafasi ya kuwa
bingwa.
Lakini
ni gharama kubwa. Tumeona msimu uliopita, timu zilishafika kwenye kituo na bado
mechi zikaahirishwa. Hii ilisababisha zitumie fedha zaidi, jambo ambalo si
sahihi.
TPLB
na TFF hawawezi kuingia hasara yoyote na wanajua timu husika lazima itasubiri.
Lakini si sahihi, zinapaswa kujua timu zinapocheza, ndiyo TFF na TPLB
zinatambulika na kuweza kujiendesha. Hivyo lazima zijenge utamaduni wa
kuzisaidia klabu, angalau kwa kuwa na mpangilio mzuri utakaowezesha
kuzipunguzia gharama zisizo rasmi.








0 COMMENTS:
Post a Comment