Na Saleh Ally
KUNA
mjadala mkubwa sana kuhusiana na suala la ushirikina michezoni na hasa kwenye
soka. Kwamba kila timu imekuwa ni lazima iende kwa mganga kwa ajili ya
ushirikina ili iweze kushinda.
Hili
linafanyika hadi katika timu za mchangani, jambo ambalo mara zote nimekuwa
nikilikemea na kuliita miradi ya wajanja wachache.
Najiuliza
mara kadhaa, kwamba vipi timu zinaamini suala la ushirikina ni lazima? Kwani
hakuna ambaye amewahi kulijengea hoja za msingi kwamba si lazima lifanyike na
kuna mara kadhaa halikufanyika na timu zikashinda?
Niliwahi
kuvuliwa unahodha nikiwa nacheza madaraja ya chini, kisa nilikataa kushiriki
kwenda kwa mganga. Mwisho timu ikafungwa mabao 4-2. Mechi iliyofuata,
hatukwenda kwa mganga, tukashinda. Ndiyo maana naona ushirikina, ni miradi ya
watu fulani.
Nilishtushwa
baada ya hivi karibuni kuzagaa mitandaoni kwa picha za video zikiwaonyesha
wachezaji wa Coastal Union wakiwa ufukweni wakishiriki masuala ya ushirikina.
Wachezaji
hao, wengine maarufu walionekana kwa sura zao waziwazi wakiwa wametulia na
mganga yuko katikati yao akifanya kazi ya kuzika kitu, sijui ni kiumbe au
tunguri!
Baadhi yao
wanasisitiza, “zika zika”. Kuonyesha kwamba ni jambo walilolizoea. Mganga naye
anafanya kazi yake huku wachezaji hao wakiendelea na stori za kawaida. Ajabu
zaidi, wachezaji hao wamevaa jezi za rangi nyekundu na nyeupe ambazo huvaliwa
na Coastal Union, tena wakiwa na furaha tele!
Kwanza
ikanishtua, kumbe kwa mganga wachezaji wanatakiwa kuvaa sare kama wanakwenda
uwanjani au wako safarini! Swali langu la msingi likawa hivi, sasa mbona
wachezaji nao hawakatai kwenda kwa mganga?
Inawezekana
pia wanapenda? Au wanaamini masuala hayo ndiyo maana nao wanaingia kwenye
kashfa hizo za ushirikina, maarufu kama “kupigana” misumari?
Swali
lililofuata, kama Coastal Union wanakwenda kwa mganga namna hiyo, iweje Ligi
Kuu Bara msimu uliopita iliisha wakipigania kuokoka kuteremka daraja? Mganga
wao hakuwa mkali, hivyo msimu ujao watabadilisha?
Najua
Yanga, Simba na timu nyingine za ligi kuu zinakwenda kwa waganga lakini kuna
kila sababu watu walio timamu kiakili waamke na kuanza kupambana na tabia hizi
za kizamani ambazo zinatufanya tuendelee kubaki tulipo.
Mafanikio
makubwa ya soka yako Ulaya, hatusikii suala la waganga au uchawi ili watu
washinde au kufanya vizuri badala yake wanapambana vilivyo kuhakikisha
kinachofanyika kinakuwa kina uwezo.
Mazoezi ya
kutosha, malipo mazuri, matunzo kwa wachezaji, vifaa bora vya maandalizi na
baada ya hapo ni juhudi na maarifa.
Tabia ya
kuabudu ushirikina ni kujikwamisha na haina maana yoyote katika ushindi. Najua
kama timu ikifungwa, mganga atawaambia hamkufuata masharti yake, ambalo ni jibu
rahisi na la kipuuzi kabisa.
Sasa
wachezaji mbona hamuachi kwenda kwa waganga kama mnaamini uwezo wenu na
maandalizi mliyofanya ya kutosha? Si sahihi na aibu kubwa wachezaji wakubwa
kwenda kwa waganga mkiwa mnaonyesha kiasi gani imani zenu haziendani na
wachezaji mnaotaka kuwa kama wao, yaani kina Cristiano Ronaldo, Lionel Messi,
Paul Pogba na wengine.
Katika
klabu karibu zote kongwe, kuna ujanja unafanyika wa watu kusingizia kuwa
waganga ni msaada. Kumbe ni miradi ya baadhi ya wanachama ambao wamekuwa
wakipewa fedha kila mechi kwenda kwa waganga.
Kama ni
hivyo, basi timu ziache kufanya mazoezi halafu waganga waamue matokeo. Au
ziachane na kununua wachezaji wazuri ili kutoa nafasi kwa waganga kufanya kazi
ili zipate ushindi na mafanikio.
Video ya
Coastal Union wakiwa kwa mganga inaonyesha kiasi gani safari ndefu iliyo mbele
ya mchezo wa soka hapa nyumbani. Lazima tubadilike, tupite njia sahihi
wanayopita wenzetu. Huku sasa imetosha.








0 COMMENTS:
Post a Comment