BUSUNGU |
Straika wa Yanga, Malimi Busungu, amepewa programu mpya ya mazoezi na kocha mkuu wa timu
hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Kabla ya mechi ya jana, Busungu alikuwa tayari ameshaifungia Yanga
mabao matatu na kuwafunika washambuliaji wenzake Mrundi, Amissi Tambwe na
Mzimbambwe, Donald Ngoma waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri
katika michuano hiyo ambayo inaendelea kutimua vumbi jijini Dar es Salaam.
Busungu amesema kuwa licha ya kiwango cha juu alichokionyesha
katika mechi mbili za mashindano hayo ya Kombe la Kagame alizoitumikia klabu
hiyo kabla ya mchezo wa jana, Pluijm amedai kuwa bado hajawa sawa kama
anavyotaka awe.
Alisema kutoka na hali hiyo, kocha huyo ameamua kumpatia programu
maalumu ya mazoezi ambayo atakuwa akiifanya kila siku baada ya mazoezi na
wenzake ili aweze kuwa katika kiwango hicho anachotaka.
“Namshukuru Mungu kwa mafanikio hayo kidogo niliyoyapata lakini
bado nina kazi kubwa ya kufanya na hivi karibuni kocha kaniambia kuwa natakiwa
kuwa fiti zaidi ya hivi nilivyo sasa kwani bado sina nguvu za kutosha kupambana
na mabeki.
“Kutokana na hali hiyo, amenipangia muda maalumu ya mazoezi
binafsi ya gym ambayo nitakuwa nikiyafanya kila siku jioni baada ya mazozi na
wenzangu kwa kipindi cha miezi mitatu na mpaka sasa nina kama siku nne tangu
nilipoanza programu hiyo,” alisema Busungu.
Busungu amejiunga na Yanga hivi karibuni kwa dau la shilingi
milioni 25 akitokea Mgambo JKT ya Kabuku mkoani Tanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment