Beki tegemeo wa Azam FC, Pascal Serge Wawa, raia wa Ivory Coast,
amezitazama timu zote zinazoshiriki michuano ya Kombe la Kagame na kutamka
kuwa, kama si timu yake ya Azam FC, basi ubingwa utabebwa na Yanga au Gor
Mahia.
Michuano hiyo imefikia hatua ya robo fainali ambayo itaanza kesho
Jumanne.
Mpaka sasa, Gor Mahia wamecheza michezo miwili na kufunga mabao
matano, hivyo wanaonekana wana njaa na ubingwa huo. Yanga wao walianza kwa
kipigo katika mchezo wa kwanza, lakini bado wana matumaini ya kufanya vizuri.
Beki huyo aliyetokea Al Merreikh ya Sudan, amesema kuwa, Yanga na Gor Mahia wanaonekana kuwa na upinzani mkubwa na wanacheza kwa
kasi na malengo. Alisisitiza kama wataendelea na moto huo, wana nafasi kubwa ya
kuchukua ubingwa.
“Mashindano bado ni magumu, sisi tumeshinda na tuna nafasi ya
kupata mafanikio makubwa ya kupata ubingwa, ingawa ni mapema kusema hivyo.
“Ukiachana na sisi, naziangalia Yanga na Gor Mahia kama timu
tishio. Zina wachezaji wazuri na zinacheza kwa malengo. Hakika kama watakuwa na
kasi hii waliyoanza nayo, wanaweza kufanikiwa kuchukua ubingwa,” alisema Wawa.
0 COMMENTS:
Post a Comment