Na Saleh Ally, Kartepe
JUZI tulifanya safari kutoka katika eneo la
Kartepe hadi Istanbul na kukutana na Watanzania mbalimbali wanaoishi hapa
Uturuki.
Kambi ya Taifa Stars ipo mlimani kabisa, katika
eneo liitwalo Kartepe ambalo limo ndani ya Mkoa wa Izimir ambao ni wa tatu kwa
ukubwa nchini hapa.
Nilishangazwa kusikia Watanzania wakifuatilia kwa
karibu kabisa kuhusiana na usajili wa timu zetu za nyumbani hasa Yanga, Simba
na Azam FC ambazo zinajulikana zaidi.
Wanajua mambo kadhaa kuhusiana na Mbeya City,
Mwadui FC, Stand United na nyingine, hakika mitandao inasaidia katika upashaji
habari hasa kwa watu wa nje.
Katika majadiliano hayo, ndipo nilikumbuka namna
ambavyo Simba imekuwa ikisumbuka kupata straika kwa njia ya ‘fasheni’, jambo
ambalo naona kabisa limepitwa na wakati.
Maswali mengi nimekuwa nikijiuliza, huenda ndiyo
wakati wa kuyaweka hapa tusaidiane kupata jibu kwenye Hoja Yangu.
Hawa Simba ni lazima wasajili mshambuliaji kutoka
nje? Wanataka kusajili straika harakaharaka, hivi kweli timu kama Simba
walikuwa hawajui wanahitaji mshambuliaji hadi wacheze mechi za kirafiki kwanza?
Nikazidi kujiuliza, kweli Simba wamekosa kabisa
straika nyumbani Tanzania au wanafanya hivyo kwa kuwa lazima wasajili mgeni ili
kuendana na Yanga kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki na wanachama wao tu? Au
wanahofia kuonekana wamefulia na wenzao Yanga na Azam FC wana mkwanja sana si
kama wao?
Hakika sehemu ya kupata majibu huenda ni kwa
Simba wenyewe, lakini nakuhakikishia ukikutana na kiongozi yeyote, maelezo
yatakuwa mengi kuliko jibu sahihi na kitu kibaya zaidi, lawama ndiyo zitachukua
nafasi kubwa kwa kuwa siku zote, viongozi wa soka hawataki kuingiliwa kwenye
njia zao na mara zote ni watu wa lawama tu!
Mimi niliona wamekuwa na haraka sana kupoteza
fedha zao za nauli kumsafirisha wakala raia wa Cameroon kuja Dar es Salaam
kufanya biashara kichaa ya kumuuza mshambuliaji Mamadou Niang ambaye baada ya
dakika 45, Simba wote hata wasio na utaalamu au uzoefu na soka, wakaona
anacheza makida.
Baada ya hapo, haraka Simba ikabeba mshambuliaji
mwingine, Abdoulaye Nd’aw naye huku tukielezwa ni hatari sana na Kocha Dylan
Kerr anamjua vilivyo!
Jibu la mapendekezo ya kocha limekuwa likitumika
sana, lakini najiuliza hivi, hayo mapendekezo yanaangalia pia kuna suala la
gharama kwa kuwa utekelezaji wake unaonekana ni ule unaoiingizia Simba gharama
zisizo na lazima na kila mara linafeli.
Kimsingi, Simba hata hawakustahili kwenda
Cameroon na Senegal, sijui baadaye Mali au kokote watakapoona. Hatua chache,
ikiwezekana kwa Bajaj tu hadi Tabata, wangegonga mlango wa Jerryson John Tegete
maarufu kama Jerry na kumueleza maneno haya: “Tunataka uchezee Simba.”
Kama angekubali, basi walikuwa na kila sababu ya
kumuweka chini na kumueleza matatizo ambayo yamesababisha ashuke kiwango. Kila
mtu anajua kuwa kuna hadithi kwamba Jerry “hayuko siriaz”.
Kuna wanaosema kwamba Jerry anaendekeza starehe
ndiyo maana ameangukia hapo. Inaweza kukawa na ukweli au kinyume chake, lakini
tukumbuke Tegete ni binadamu, anaweza kubadilika kutokana na mazingira.
Kwani nani anajua Tegete amejuta mara elfu ngapi
baada ya kuachana na Yanga? Nani anajua sasa anataka kuonyesha nini na kurudi
wapi?
Nasema Tegete kwa kuwa Watanzania wote tunajua
ana uwezo kisoka tena ni mshambuliaji akikutana na nyavu za taifa, zinajua
Tegete anakuja tena.
Kwa maana ya uwezo wake hakuna mwenye hofu,
kilichopo ni matatizo yaliyoingia katikati na Simba wangeyamaliza hayo, basi
wangempa mkataba mfupi wa mwaka mmoja.
Wakamlipa mshahara mzuri, wakamlipia nyumba bomba
na kumpa posho safi. Hakika angefanya vema huku akiwa na lengo la kuwaonyesha
Yanga kuwa anaweza.
Tangu Simba ilipompoteza Amissi Tambwe kwa kujua
kwingi, imekuwa ikihaha kila kukicha kuziba pengo hilo ililolitengeneza kwa
makusudi, lakini ajabu, inaamini nje tu.
Nafikiri ubunifu uingie kwenye vichwa vya
wanaoshughulikia usajili nchini, wakati mwingine wafanye mambo yanayoeleweka na
si hizo hadithi za kina Niang, eti kaka yake ni yule straika hatari wa Senegal
aliyeitesa Stars. Aaah!
0 COMMENTS:
Post a Comment