August 28, 2015


Na Saleh Ally
HIVI karibuni niliandika makala kuhusiana na kushangazwa na Simba kutaka kumsajili kipa mwingine wakati wana Ivo Mapunda, Peter Manyika pamoja na makipa wengine makinda.


Nilijaribu kuwakumbusha, kama watakuwa na kipa wa kigeni, Ivo na Manyika, basi kulionyesha dalili zote za kumpoteza kipa huyo kinda.

Pia nikawakumbusha Simba kwamba wamekaa muda mrefu na kijana huyo, amewaumiza mara nyingi kutokana na makosa yake.

Kila anayekua lazima anafanya makosa, hasa kama kazi bado hajaizoea vizuri lakini kama wewe una nia ya kuendelea lazima ujifunze kupitia yale makosa ili ukue kiutendaji.

Niliona msimu huu, ungekuwa wa kukua kwa Manyika kwa kuwa angepata nafasi ya kuyafanyia kazi makosa yake na kuzidi kukua kiutendaji. Hivyo kuongeza makipa tena wakongwe wawe wawili, ingekuwa ni kukubali afe kimpira.



Simba wakafanya hivi, wakaachana na Ivo wakidai alikuwa akiwaletea “mapozi nami” ingawa mwenyewe alikanusha hilo. Halafu wakamsajili kipa kutoka Ivory Coast.

Kwa hapo, bado sioni kama kuna tatizo kama kipa huyo mgeni atakuwa bomba na uwezo wa juu. Halafu bado Manyika akapewa nafasi zaidi ya kucheza. Tanzania inamhitaji Manyika na inahitaji makipa wenye vipaji na yeye ameonyesha kwa kuwa baba yake alishaonyesha, basi hakuna anayeweza kuwa na hofu naye.

Manyika ni kinda, lakini tukubali katika umri wa chini ya miaka 21 lazima anahitaji usimamizi wa karibu. Baba yake, Manyika Peter, ameeleza namna ambavyo amekuwa akijitahidi kumshauri.

Lakini bado, Manyika anahitaji usimamizi wa karibu, mtu atakayemueleza ukweli na pia kumnyooshea njia sahihi ya kupita.

Mwishoni mwa msimu uliopita alionyesha kiwango kibovu kabisa na taarifa zikaeleza kwamba kuna mrembo ‘kamkoleza’ hivyo kumfanya ashindwe kuwekeza akili zake kwenye soka. Kwani alikuwa akimfuata hasa mazoezini, jambo ambalo mchezaji anayejitambua hawezi kulifanya.

Mara mrembo huyo akaanza kutupia picha rundo kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wanabusiana na vinginevyo. Halafu alipoanza kuulizwa na waandishi akafuta huku akisisitiza ni rafiki yake tu.

Sasa safari hii mwanadada huyo ambaye nimeelezwa anamzidi umri Manyika amekuwa akiweka picha wakiwa wamekumbatiana huku akiandika maneno kadhaa ya mapenzi kuonyesha kiasi gani wanapendana zaidi.

Kingine kibaya zaidi, anaonekana yeye ni shabiki wa chama kimoja cha siasa. Hivyo sasa anamjumlisha Manyika sijui na mwenyekiti wa chama hicho, mara akiwa na makada wenzake, jambo ambalo si sahihi kwa Manyika.

Manyika ana haki ya kuchagua chama chochote, basi ni vema kufanya mambo kwa utaratibu na si kuonyesha hana la kusema, hatambui kuwa mashabiki wa klabu anayoichezea ni wanachama wa karibu vyama vyote vya siasa.

Wakati mwingine si vizuri kuonyesha ushabiki hadharani wa chama gani. Jambo hilo linaweza kujenga chuki kati yake na mashabiki hasa ikifikia siku amekosea. Soka ni mchezo wa lawama kwetu Tanzania.

Akumbuke yeye si msanii wa hip hop, picha zake akionekana amekumbatiwa, anapigwa busu, bado si jambo sahihi hata kama ana uhuru. Watu wanaomuangalia Manyika ni wengi wakiwemo vijana chini yake ambao kama wataona anafanya lolote bila kuonekana si sahihi, mwisho wataiga halafu tutatengeneza kundi la vijana wanaojipamba kwa ‘mibusu’ mitandaoni ambayo si mwenendo sahihi wa soka.

Wachezaji kibao wa Ulaya, Afrika na kwingineko wana akaunti za Instagram, Facebook na mitandao mingine ya kijamii. Anaweza kujifunza.

Simba ni taasisi kubwa, anayeitumikia lazima ajitambue kwa kila anachofanya kama hakigusi au kuharibu heshima ya klabu hiyo. Kuangalia kama hakuna athari kwa klabu kwa chochote anachokifanya lakini kujilindia hadhi pia ni jambo jema. Kaeni karibu na Manyika msaidieni, naye asikilize lakini kama atalazimisha mwenendo huu. Basi safari yake haitakuwa ndefu.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic