August 1, 2015


Michuano ya Vilabu Bingwa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) inatarajiwa kufika tamati kesho jumapili katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kwa mchezo wa Fainali utakaozikutanisha timu ya Azam FC dhidi ya Gor Mahia.


Viingilio vingine vya mchezo huo wa kesho wa fainali ke ni VIP A ni shilingi elfu kuni na tano (15,000) na VIP B & C, Shilingi elfu kumi (10,000) na sehemu nyingine ya uwanja  iliyobakia ni shilingi elfu tatu (3,000) kwa viti vya rangi ya bluu, kijani na rangi ya chungwa.

Katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika jana, Gor Mahia iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3- 1 dhidi ya Khartoum mabao yaliyofungwa na Michael Olunga, Innocent Wafula na Kagere Meddie na kukata tiketi ya kucheza fainali.

Gor Mahia chini ya kocha wake Frank Nuttal mpaka kufikia hatua ya fainali, imecheza jumla ya michezo sita, ikiwemo michezo minne katika hatua ya makundi, robo fainali na nusu fainali, ambapo imeweza kushinda michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja.

Mshambuliaji wa Gor Mahia,Michael Olunga anaongoza kwa ufungaji, akiwa amepachika mabao matano, akifuatiwa na nahodha wa Khartoum Salehdin Osman na msadizi wake Amin Ibrahim wote wenye mabao manne kila mmoja.

Kwa uapnde wa Azam chini ya kocha wake Stewart Hall, imefanikiwa kufika hatua ya fainali bila ya kuruhusu nyavu zake kutikisika, huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa imepachika mabao tisa (9) katika michezo mitano iliyocheza kuanzia hatua ya makundi.

Kuelekea mchezo wa Fainali, Azam FC iliziondosha Yanga SC kwa mikwaju ya penati (5-4) hatua ya robo fainali, na kasha kuindoa KCCA hatua ya nusu fainali kwa kuifunga kwa bao 1- 0, bao lililofungwa na mshambuliaji chipukizi Farid Musa.
Mshambuliaji Kipre Tchetche ana mabao matatu kwa upande wa washambuliaji wa Azam FC, akifuatiwa na nahodha John Bocco na Farid Musa wenye mabao mawili kila mmoja.

Katika fainali hiyo ya kesho, inatarajiwa kuwa ya vuta ni kuvute kutokana na makocha wa timu hizo, Frank Nuttal wa Gor Mahia kutaka kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 tangu Gor Mahia kushinda kombe hilo mara ya mwisho mwaka 1985 walipotwaa kwa mara ya tano (5).

Huku Stewart Hall akiwania kuweka historia ya kwanza kwa klabu ya Azam FC kuweza kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo miaka tisa iliyopita, baada ya kusindwa kutwaa taji hilo ilipotinga fainali mwaka 2012 kwa kufungwa na Yanga SC mabao 2-0.

Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuanza saa 9:45 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, huku mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ukitarajiwa kuanza saa 7:30 mchana ukizikutanisha timu za Khartoum ya Sudan dhidi ya KCCA kutoka nchini Uganda.

Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa kitita cha Dola za Kimarekani Elfu Thelathini (U$ 30,000), mshindi wa pili Dola za Kimarekani Elfu Ishirini (U$ 20,000) huku mshindi wa tatu akizawadiwa Dola za Kimarekani Elfu Kumi (U$ 10,000).

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini Mkoa wa Temeke, linawashikilia watu watatu  kutoka nchini Kenya kufuatia kufanya kosa la shambulio katika mchezo wa nusu wa fainali kati ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Raia hao wa Kenya walifanya shambulio kwa mlinzi wa TFF uwanja wa Taifa, Omary Mayai wakiwa katika jukwaa la VIP A ambapo askari polisi walijaribu kuwaonya na kuwaomba kuwa wastaarabu, lakini walishidwa kutii amri ya polisi na kuendelea kufanya vurugu kabla ya mmoja wao kukimbilia ndani ya uwanja na kuketi katika benchi la ufundi la Gor Mahia.


Namba ya jarada la kesi iliyofunguliwa kituo cha Polisi cha Chang’ombe ni CHA/RB6265/2015, na wanaoshikiliwa kituoni hapo ni mshabiki wa Gor Mahia Jackson Mjidie (Jaro Soja), pamoja na waandishi wa habari wawili kutoka kituo cha Citizen, Okinyi Mike na Jariri Otieno.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic