Na Saleh Ally
NIMEKUWA nikizungumzia sana kuhusiana na
suala la Simba kulipwa zile fedha dola 300,000 (sasa Sh milioni 600),
walizomuuza mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi kwa Etoile du Sahel ya Tunisia.
Nirudie leo kwenye kukumbusha kwamba,
biashara ya kumuuza Okwi kutoka Simba kwenda Etoile ilikuwa ni ya kisanii,
haikuwa ya kitaalamu, waliohusika pia hawakuwa watu makini hata kidogo.
Nimekuwa nikisisitiza hilo tangu siku ya
kwanza biashara ilipofanyika, nikaeleza inaonyesha wazi kuna mianya mingi ya
Waarabu hao kutolipa fedha hizo.
Lakini nilisisitiza tena baada ya Okwi
kurejea nchini na kuanza kuichezea Yanga. Bahati nzuri Etoile ikaja nchini
kucheza na Yanga, nikafanya mahojiano na bosi wa Etoile pamoja na Shirikisho la
Soka Tunisia (FTF).
Matamshi yao, yalionyesha wazi hakukuwa na
mpango wa kulipa fedha hizo, mmoja alisema: “Simba wanataka fedha ya nini
wakati Okwi yuko hapa anaichezea Simba?” Pia nikalieleza hilo.
Inawezekana Simba ikalipwa kwa kuwa
imelifikisha suala hilo kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa),
tukaelezwa limetoa agizo kuwa wawalipe Simba haraka. Hadi leo bado, sijajua
haraka inachukua kipindi gani.
Jaribu kuangalia hili, Simba ilimrejesha
Okwi akitokea Yanga. Pamoja na tafrani zilizotokea, alifanikiwa kubaki Msimbazi
na kuitumikia kwa ufanisi mkubwa kwa msimu mmoja.
Baada ya hapo, kupitia makubaliano ya kila
upande, Simba ikamuuza Okwi Denmark katika Klabu ya Sonderjyske kwa Sh milioni
120, safari hii hakukuwa na longolongo.
Kwanza baada ya Wazungu hao wa Ulaya
Kaskazini kuweka ahadi, Simba waliendelea kubaki na haki za mchezaji huyo kwa
maana ya uhamisho na malipo yalipofanyika, Okwi akawa huru kuitumikia timu yake
mpya.
Kidogo hapa unaona tofauti kubwa kati ya biashara
ile ya kwanza na hii. Simba walibaki na haki za Okwi, kwamba hawakufanya
uhamisho wa kimataifa wakisubiri kulipwa. Lakini mauzo kwenda Etoile, aliyekuwa
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisisitiza uhamisho ufanyike tu.
Nikaibuka nikasema Simba imemuuza Okwi
‘bure’ na hilo ndilo linaloendelea kuthibitika hadi leo, licha ya ubishi mwingi
na kuzuka kwa makundi kwamba namsakama Rage.
Nilitamani sana Simba ilipwe ili Simba na
wale waliokuwa mashabiki wa uongozi uliopita walioutetea kwa kufanya upuuzi huo
katika mauzo, waweze kunisema. Lakini binafsi ningenyamaza kimya na kujipongeza
kwa kuanzisha presha iliyochangia wao kuchangamka na kufanikisha malipo.
Lakini sasa bado roho inaniuma kuona klabu
kutoka katika nchi niliyozaliwa na kukulia inadhulumiwa fedha Sh milioni 600,
tena kijinga kabisa huku sababu zisizo na mashiko zikitolewa kutaka
kuwalainisha Wanasimba.
Inavyokwenda, Simba watafikia watakaa kimya
tu na kuachana na fedha hizo zipotee. Ni ahadi inayorudi nyuma badala ya kwenda
mbele.
Badala ya kutumia kanda kusikiliza muziki
huo, sasa tutoke kwenye kanda hizo maarufu kama kaseti na twende kwenye CD.
Fedha zile si za Rage, si za Zacharia Hans
Poppe, si za Saleh Ally ni za Wanasimba. Usisahau wenye fedha hizo ni
Watanzania na ndiyo maana ninakuwa nina haki ya kuhoji na nitaendelea kutumia
ujinga huu wa Simba kama sehemu ya mfano katika muda wangu wote wa maisha ya
uandishi wa habari.
Nitawakumbusha viongozi wengine kutorudia
upungufu mkubwa wa umakini uliofanywa na Rage halafu baadaye wakajaribu
kuutetea na kutaka kulazimisha ionekane kama wanadharauliwa au kuonewa ili wapate
watu wasio waelewa waweze kuwatetea ili nionekane sina nidhamu kudharau
wakubwa. Nasisitiza, kuna kila sababu ya kutofautisha kuelezana ukweli na
heshima, sijawahi kumdharau mtu.
Rage kaboronga, sasa wote tukae kimya au
tuunge mkono alichokifanya? Ukweli hauna mwenyewe, ukimwagwa kwenye mchanga,
kamwe haukauki na hilo ndilo linaloendelea kubaki.
Usisahau Simba imetumia fedha nyingi sana
ikiwa ni juhudi ya kutaka kulipwa fedha hizo. Gharama zimekwenda juu sababu tu
ya umakini uliokosekana siku ya mauzo.
Niongeze kidogo, inapofikia suala la hoja za
msingi, basi tuache ushabiki. Hata kama utakuwa na urafiki na aliyekosea, basi
msaidie kwa kumueleza ukweli, upambe si jambo jema katika maisha ya mwanadamu
imara.
Simba inaendelea kudai fedha za Okwi katika
biashara ya miaka mitatu iliyopita, wakati tayari imeshalipwa kwenye biashara
ya Okwi ya mwaka huu, kichekesho!
0 COMMENTS:
Post a Comment