Na Saleh Ally, Kartepe
TAKRIBANI wiki moja na siku moja niko hapa kwenye mji mdogo wa
Kartepe nchini Uturuki ambako timu ya taifa ya soka, Taifa Stars imeweka kambi
yake.
Taifa Stars inajifua hapa Uturuki kwa kuwa inataka kutimiza jukumu
la kuinyoa Nigeria katika mechi ngumu ya kuwania kucheza Kombe la Mataifa
Afrika (Afcon).
Nigeria si timu ndogo, inatoka katika nchi tajiri zaidi ya
Tanzania na hata Shirikisho lake la Soka (NFA), ni tajiri sana kuipita TFF.
Lakini TFF imejitutumua kupitia wadhamini wake, Bia ya Kilimanjaro
na kufanikiwa kuiweka Stars katika kambi nzuri kabisa ambayo klabu yoyote ile
ya soka ingejiona ipo katika sehemu sahihi kwa ajili ya kambi ya maandalizi.
Vifaa vizuri vya mazoezi, mfano viwanja bora na hata mipira.
Chakula na sehemu ya kulala ni bora zaidi. Lakini hali ya hewa ya baridi
isiyoumiza, pia inachangia wachezaji kujifua katika kiwango ambacho ni bora
kabisa.
Lengo ni kuitoa Nigeria, Watanzania wengi sasa watakuwa na
matumaini kutokana na taarifa hizo za maandalizi.
Mfano mzuri wa maandalizi mazuri ni namna Stars ilivyocheza katika
mchezo wake wa kirafiki wa mazoezi dhidi ya Libya uliochezwa katika moja ya
viwanja vya hoteli waliyofikia.
Stars walionyesha wako vizuri licha ya makosa kama vile kwenye
safu ya ulinzi, wakati mwingine kiungo kulala lakini pia kushindwa kuichezesha
vilivyo safu ya ushambuliaji.
Kocha Mkuu, Charles Boniface Mkwasa ana matumaini ya kikosi chake
kurekebisha yale waliyoyaona na ameahidi zaidi watauchezea mpira na Stars sasa
itafanya mazoezi mara moja kwa siku ili kuepusha kuwachosha kwa kuwa mechi
imekaribia.
Wakati Stars itakaporejea nyumbani Tanzania, usiku wa kuamkia
Jumatano na kuanza maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kuivaa Nigeria, Watanzania
lazima wajue wao ni sehemu ya ushindi.
Nigeria ni timu bora kuliko Tanzania kama tutazungumzia maana ya
uzoefu wa michuano mikubwa, lakini wenzetu wana wachezaji wengi wanaocheza soka
katika nchi zilizoendelea kisoka, lazima watakuwa na mengi zaidi yetu kama silaha.
Wanajua wanakuja kucheza na timu ambayo kamwe hawataidharau, hivyo
watapambana kwa kila namna, lakini si kweli kwamba hawafungiki.
Tanzania imejiandaa na kikubwa kinachoweza kuitofautisha na
Nigeria ni kwamba inacheza nyumbani. Tofauti hiyo haiwezi kuwa jina la uwanja
au jina la mji.
Sheria ni zilezile 17 za soka, hivyo bado hakuna tofauti. Kikubwa
kinachowatofautisha Tanzania na Nigeria
ni kwamba, Taifa Stars itakuwa na mashabiki wengi wanaoishangilia. Hao
ni mimi na wewe kwa maana ya utaifa wetu.
Hapa ndipo ilipo hoja yangu ya msingi kwamba Watanzania wajitokeze
kwa wingi sana uwanjani siku hiyo kuishangilia Stars. Wajue wao wanaweza kuwa
mchango mkubwa na wakagawana umuhimu na kambi ya Uturuki ambayo imetumika kwa
maandalizi ya Stars.
Unajua ule msemo kwamba shabiki ni mchezaji wa 12 na ndiyo maana
ya timu kucheza ugenini. Jitokezeni kwa wingi kuishangilia Taifa Stars na
kuizomea Nigeria.
Mnajua kabisa katika soka kuna makosa, msitegemee kuona Stars
inacheza dakika 90 bila makosa. Uvumilivu kwa timu yenu, kuwavunja Nigeria moyo
tena kwa juhudi zote ndiyo kazi yenu.
Isitokee kundi dogo la mashabiki wa Nigeria wajitokeze uwanjani na
kuanza kuwafunika zaidi ya mashabiki 40,000 au zaidi watakaokuwa pale. Lazima
nao wajue kweli kwamba wako ugenini. Nyumbani kwa Taifa Stars.
Leo nimeamua kuzungumza na mashabiki, siku chache zijazo itakuwa
zamu ya wachezaji niwaeleze nilichokiona Uturuki na ushauri wangu juu yao wafanye
lipi.
0 COMMENTS:
Post a Comment