Kipa mpya wa Mbeya City ya jijini Mbeya, Juma Kaseja, ameibuka na
kuipa mbinu timu yake hiyo kwa kusema kuwa ili waweze kufanikiwa kufanya vyema
msimu ujao, wanahitaji kuunganisha nguvu zao pamoja, kuanzia wachezaji, benchi
la ufundi na mashabiki wa timu hiyo.
Kaseja amesajiliwa Mbeya City hivi karibuni kwa mkataba wa miezi
sita kwa dau la shilingi milioni sita ambapo mchezaji huyo hakucheza ligi yote
msimu uliopita, baada ya kuondoka Yanga.
Kaseja alieleza kuwa, ujio wake katika timu hiyo siyo kuwa ndiyo utamaliza
tatizo kwa kuisaidia timu hiyo kufanya vyema, kwani timu haichezwi na mchezaji
mmoja kisha kuleta mafanikio na kudai kuwa ushirikiano ndiyo utakaoisaidia
kujiweka vizuri.
“Timu haichezwi na mtu mmoja, bali inachezwa na watu wote, siyo
kuja kwangu ndiyo kutamaliza kila kitu, isipokuwa kinachotakiwa ni ushirikiano
kuanzia wachezaji, viongozi pamoja na mashabiki wote wa Mbeya City.
“Hata akiletwa Messi (Lionel) kuja kucheza kutokana na ubora wake,
hawezi kufanikiwa bila ya kuwa na ushirikiano wa kutosha na wachezaji
aliowakuta.
“Hivyo naamini tukishirikiana kwa pamoja tutaisaidia timu yetu kuweza
kufanya vyema msimu ujao,” alisema Kaseja.
0 COMMENTS:
Post a Comment