Kweli Yanga imepania kutetea kombe lake, kwani zikiwa zimebaki
siku 12 kabla ya Ligi Kuu Bara kuanza kutimua vumbi, Kocha wa Yanga, Mholanzi,
Hans van Der Pluijm, ameamua kuifungia kazi safu yake ya ushambuliaji baada ya
kuridhishwa na mabeki katika mechi kadhaa za kirafiki walizocheza.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga, inaongozwa na mastraika watatu
matata; Malimi Busungu, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
Yanga inatarajia kuanza ligi kuu kwa kuvaana na Coastal Union ya
Tanga katika Uwanja wa Taifa ambapo hadi sasa imeshacheza mechi kadhaa za
kirafiki na kutofungwa.
Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimeeleza kuwa, Pluijm yupo
katika mpango wa kuhakikisha anawanoa washambuliaji wake katika suala zima la
umaliziaji kutokana na safu hiyo kuonekana kuwa na tatizo kwenye umaliziaji.
“Timu inajiandaa na ligi ambapo kocha Pluijm ameamua kuanzisha
programu maalumu kwa ajili ya kuwaweka fiti washambuliaji kwa kufanya ‘effort’,
kwani timu imekuwa ikishambulia kwa masaa mengi na kwa harakaharaka bila ya
kufunga, hivyo kwa sasa ndiyo kazi anayoifanya.
“Kwa upande wa safu ya ulinzi, ameridhika nayo kutokana na timu
kutofungwa katika mechi nyingi za kirafiki tulizocheza, isipokuwa kuna makosa
madogomadogo yanayohitaji kurekebishwa kabla ya ligi kuanza.
“Ameeleza kuwa anahitaji wachezaji aliobaki nao waweze kuimarika
zaidi kwa kuwa ana imani kuwa waliokuwa katika timu za taifa wakirejea watakuwa
fiti,” kilisema chanzo hicho.
Straika aliyeifungia Yanga mabao 13 kwenye
Ligi Kuu Bara msimu uliopita, amezungumza na Championi Jumatatu akiwa Burundi
alikokwenda kwa ajili ya kuitumikia timu yake ya taifa. Amesema Pluijm
aliwaambia mastraika wote msimu ujao anataka ashuhudie mabao ya kutosha.
“Kwa
sasa nipo Burundi na timu yangu ya taifa ila kuna jambo ambalo kabla ya kuja
huku, kocha Pluijm alituambia washambuliaji wote kwamba tuongeze umakini kwani
hafurahishwi kabisa na idadi ya mabao tunayofunga kwa sasa.
“Kutokana na hali hiyo, ametuambia kuwa, kila
mshambuliaji anatakiwa kuwa makini na kucheza soka kwa faida ya timu na faida
hiyo ni kufunga mabao mengi, jambo ambalo anaamini kabisa kuwa tunaweza
kulitekeleza,” alisema Tambwe.
Tangu Yanga ilipoanza maandalizi yake ya
kujiandaa na msimu ujao wa ligi kuu kwa kucheza mechi mbalimbali za kirafiki na
zile za michuano ya Kombe la Kagame, safu hiyo ya ushambuliaji imeshazifumania
nyavu mara 21 katika mechi 11. Mabao 15
kati ya hayo, yamefungwa katika mechi za kirafiki.
SOURCE: CHAMPIONI JUMATATU
0 COMMENTS:
Post a Comment