August 12, 2015


Na Saleh Ally
BAADA ya mechi 26 za Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Yanga ndiyo walitangazwa kuwa mabingwa rasmi. Hata hivyo, mechi tatu kabla walishajua kuhusiana na cheo chao hicho cha Wafalme Wapya.

 Hadi mwisho kabisa wa ligi, Yanga walikuwa wameshinda mechi 17 kati ya 26 walizocheza na kuwa timu iliyoshinda mechi nyingi zaidi kwani Azam FC iliyokuwa ya pili na Simba katika nafasi ya tatu, kila moja ilikuwa imeshinda mechi 13 tu.


Ukiachana na ushindi huo ambao ulionyesha Yanga ilikuwa na kikosi imara, safu yake ya ulinzi ilifungwa mabao 18, sawa kabisa na safu ya ulinzi ya Azam FC, huku Simba katika nafasi ya tatu ikiruhusu mabao 19.

Nafasi ya nne Mbeya City iliruhusu mabao 22 na katika nafasi ya tano, Coastal Union ikaruhusu mabao 25.

 Kwa upande wa mabao ya kufunga, Yanga pia iliongoza ikiwa na 52, ikifuatiwa na Simba iliyofunga 38 na kuipita Azam FC katika nafasi ya pili ikiwa na mabao 36. Mbeya City ilimaliza na mabao 22 na Coastal Union 21.

 Utaona kitu hapo, licha ya kuwa na tofauti kubwa kati ya Yanga na timu nyingine katika ushindi wa mechi na mabao ya kufunga, hakuna tofauti kubwa katika mabao ya kufungwa.

Mabao ya kufungwa ndiyo jibu la ubora wa safu ya ulinzi ya timu husika. Kweli Yanga imekuwa na safu nzuri ya ulinzi, inayolingana na mshindi wa pili, lakini yenye tofauti ya bao moja tu na mshindi wa tatu ambaye ni Simba.

Kama utazungumzia ubora wa juu katika msimu kwa maana ya uchambuzi wa kikosi kwa eneo, safu ya ushambulizi ya Yanga ndiyo ilikuwa bora zaidi kwa msimu huo na hilo halina ubishi.

 Lakini kama ni safu ya ulinzi, Yanga inakuwa si bora zaidi lakini ni moja ya bora. Maana iko sawa na Azam FC, pia ina tofauti ya bao moja zaidi la kufungwa na Simba iliyokuwa nafasi ya tatu.
 Utaona safu ya ulinzi ya Simba iliyokuwa inaongozwa na vijana kama Juuko Murshid na Hassan Khatibu ilivyoweza kupambana na kuwa anga za safu ya ulinzi inayoongozwa na wachezaji wakongwe na tegemeo kwa taifa kama Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Kwa maana ya takwimu, kuna tofauti kubwa kati ya safu ya ushambuliaji ya Yanga msimu uliopita na ile ya Simba na vikosi vingine. Lakini hakuna tofauti kubwa kati ya safu hiyo ya ulinzi ya Yanga na Simba.

Usisahau safu ya ulinzi ya Yanga inaongozwa na mabeki wawili wakongwe na tegemeo kwa taifa letu, awa ni Cannavaro na Yondani.
Binafsi ninaamini safu hiyo ilipaswa ifanye vizuri zaidi na huenda ndiyo chanzo cha kuona imeshindwa kufanya vyema katika mechi za majaribio na sasa uongozi wa Yanga umeamua kuiongezea nguvu katika safu ya ulinzi.

Ajabu ukiwasikia watu wengi wanazungumzia matatizo ya ulinzi, zaidi wanasema kuhusiana na Yondani kwamba ameisha!

 Hakuna anayeeleza Yondani ameisha vipi, lakini kitakwimu inaonyesha wazi ambaye kiwango chake kimeshuka ni nahodha Cannavaro. Huenda suala la heshima limetangulia na inakuwa vigumu kumueleza ukweli nahodha huyo wa Yanga na Taifa Stars.

 Cannavaro ni msikivu, mnyenyekevu, mtu mzuri na mwenye nidhamu. Lakini uchezaji wake unaonyesha wazi kuwa hayuko vizuri kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita.

Mbaya zaidi, haelezwi ukweli ikionekana si sahihi kumueleza nahodha na hilo ni kosa kubwa kwa kuwa inazidi kumdidimiza.
Niliwahi kumhesabia Cannavaro, karibu msimu mzima katika mechi zilizochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mipira yote 56 ya vichwa dhidi ya washambuliaji alipiga yeye isipokuwa miwili tu dhidi ya Felix Sunzu.

Wakati Taifa Stars ilipocheza mechi ya kirafiki na kufungwa bao 1-0 na Ivory Coast, Didier Drogba aliruka mara saba juu na Cannavaro. Tembo huyo alipiga vichwa viwili na kimoja akafunga bao lakini vitano vyote alipiga beki huyo.

Lakini hivi karibuni imekuwa kawaida tu kwa washambuliaji kupiga mipira ya vichwa mbele ya Cannavaro na uliona Michael Olunga wa Gor Mahia alivyofanya.

Suala la kujipanga na kuipanga safu yake ya ulinzi limekuwa tatizo kwa Cannavaro ambaye alikuwa na uwezo mkubwa na ndiyo moja ya sifa za juu za ‘kitasa’ au namba tano. Sasa safu yake ya ulinzi inapotea njia tu na haya matatizo si ya Yondani, ni yake Cannavaro.

 Yanga imefanikiwa kuimarisha kiungo cha ulinzi kwa kumsajili, Thabani Kamusoko kutoka Zimbabwe, hili ni sahihi na awali nililieza.

Pamoja na kumsajili Vicent Bossou kutoka Mali kuimarisha ulinzi, kama Yondani atabaki nje, basi Cannavaro lazima arekebishe hayo, la sivyo itakuwa kazi bure katika safu ya ulinzi na huenda hakutakuwa na maana ya mabadiliko hayo.
Kingine nisisitize, suala la ukimya kwa maana ya heshima au kuoneana haya, halijengi. Tuache unafiki ili tuelezane ukweli kwa faida ya soka ya Tanzania.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic