Kesho Jumapili Yanga inacheza mechi ya kirafiki
na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya katika kujiandaa na msimu ujao wa
Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika kikosi cha Yanga, yumo kiungo
mshambuliaji Deus Kaseke aliyesajiliwa hivi karibuni kutoka Mbeya City, ambaye
angeweza kuutumia mchezo huo kuwaaga wachezaji wenzake.
Pengine Kaseke angecheza kipindi cha kwanza
akiwa Mbeya City kisha kipindi cha pili akacheza Yanga kama alivyofanya
Geoffrey Mwashiuya pindi timu yake ya zamani ya Kimondo ilipocheza na mabingwa
hao watetezi wa ligi kuu.
Kaseke amesema kuwa,
haoni sababu ya kuichezea Mbeya City kwani tayari yeye ni mchezaji wa Yanga na
hawezi kuichezea timu nyingine.
“Nicheze
Mbeya City? Hapana, nitacheza Yanga kwa dakika zote tena kwa kiwango changu
kilekile, watu wasitarajie kwamba nitazitumikia timu zote kwa vipindi tofauti.
Waelewe tu kuwa mimi ni mchezaji wa Yanga.
“Wachezaji wengi hasa wa kimataifa wamekuwa
wakifanya hivyo, lakini kwangu sijafikiria,” alisema Kaseke ambaye
amejihakikishia namba kwenye kikosi cha Yanga.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Mbeya City,
Juma Mwambusi, alisema: “Nilikuwa Dar es Salaam, ndiyo narudi Mbeya sasa
(jana), nitaiandaa timu kesho (leo Jumamosi) kwa mechi hiyo.”
Katika mchezo huo, Yanga inatarajiwa kuwatumia
nyota wake wengine wapya akiwemo Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Malimi Busungu,
Simon Matheo, Benedict Tinocco na Haji Mwinyi.
0 COMMENTS:
Post a Comment