August 21, 2015


Na Saleh Ally
MALAGA ndiyo timu ya kwanza katika msimu mpya wa La Liga wa 2015-16 kucheza mechi yake ya kwanza ya ligi hiyo nyumbani.


Mji wa Malaga unaosifiwa kuwa na mandhari bora kabisa katika miji mingi ya Ulaya itakuwa na ugeni wa wababe Sevilla ambao wameonyesha uwezo mkubwa katika misimu miwili iliyopita.

Licha ya kumkosa Carlos Bacca, Sevilla imeweza kuisumbua kwa kiwango cha juu Barcelona ambayo ilibeba Kombe la Super Cup ya Uefa, siku kadhaa zilizopita kwa mabao 4-3.


Uwezo waliouonyesha, sasa wanaurudisha La Liga ambako wanakutana na Malaga kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa La Rosaleda.

Kitu kizuri mashabiki wa soka kuanzia Tanzania, Uganda, Rwanda na sehemu nyingine za Ukanda wa Afrika Mashariki watapata nafasi ya kuona mechi hiyo moja kwa moja kupitia Azam TV.

Malaga na Sevilla zimekuwa na ushindani wa juu kabisa katika La Liga pia Copa del Rey, ni timu ambazo kila zinapokutana, kunakuwa na mashabiki wengi na mechi yao ya ufunguzi wa ligi, tiketi zake ziliuzwa haraka mno ndiyo maana unaweza kusema uhakika wa Dimba la La Rosaleda linalochukua watu 30,044 kujaa pomoni, hauna mjadala.

Malaga imejiimarisha vilivyo na mmiliki wake Sheikh Abdullah Al Thani amekubali kutoa fedha za kutosha ili kuhakikisha msimu ujao wanafanya makubwa zaidi.

Tayari timu hizo zimekutana mara 30 katika michuano mbalimbali ikiwemo La Liga na Copa del Rey na inaonekana zimekuwa na ushindani wa juu kabisa.

Sevilla imeshinda mara 11 wakati Malaga imeshinda mara 12 na zimetoka sare 7, huku wastani wa mabao yao ya kufunga na kufungwa ukiwa sawa kabisa.


Inawezekana pamoja na kutaka pointi tatu muhimu ili waanze La Liga vizuri lakini Sevilla watakuwa na hamu ya kusawazisha ili nao wawe wameshinda mara 12 na si kupoteza mara 13.

Kasi ya timu hizo inakupa picha kwamba hata kama hazikutani Barcelona na Madrid lakini mechi itakuwa ngumu kwa kuwa angalia ubora wa Sevilla na ilivyoisumbua Barcelona, lakini inapokutana na Malaga kazi inakuwa pevu kwake.

Aina ya uchezaji wa timu zote kama unafanana kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kweli zinacheza Spanish Football lakini zinatumia nguvu kama ile aina ya Real Madrid.

Pasi nyingi, kasi na krosi fupi ambazo zinaingia ndani ya boksi kutoka pembeni na katikati, hivyo kufanya mpira uwe na ladha zaidi ya kutazama kutokana na mvuto.

Sifa nyingine ya mechi hiyo, huenda kwa kuwa timu zote zinatumia nguvu sana, kumekuwa na rekodi ya kadi nyekundu nyingi. Mfano katika mechi 18 zilizopita kuanzia msimu wa 2005-06, kuna kadi nyekundu tisa zilipatikana, hata mechi ya mzunguko wa pili wa La Liga, Malaga ikiwa nyumbani, mchezaji wake alilambwa kadi nyekundu.

Inachoweza kujivunia Sevilla ni hivi, kwamba katika La Liga, msimu uliopita ulikuwa wake. Ilianza kushinda bao 2-0 katika mechi yake ya nyumbani lakini iliposafiri kwenda ugenini ikashinda kwa mabao 3-2.

Sasa unapozungumzia suala la ushindi kwenye Uwanja wa La Rosaleda, wageni Sevilla ndiyo wa mwisho kushinda hapo. Je, wataendelea msimu ya msimu uliopita au wenyeji watakomaa?

Hii inaonyesha kiasi gani ushindani mkubwa na unavyozidi kupanda juu dhidi ya timu hizi unavyoongeza joto katika mechi ya kesho.

Usisahau kitu kimoja, mara baada ya La Liga kumalizika msimu uliopita, kila timu ikiwa imecheza mechi zake 38 kwa timu zote 20, Sevilla ilikwama katika nafasi ya 5 ikiwa na pointi 76 huku Malaga ikiishia katika nafasi ya 9 ikiwa na pointi 50 tu.


Kwa leo kutakuwa na mechi hiyo moja tu inayofungua pazia la La Liga lakini kesho mechi nyingine nne, uhondo unaendelea ndani ya Azam TV.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic