Na Saleh Ally
VIKOSI vya Yanga, Simba na Azam FC
ndivyo vilivyosajili wachezaji wengi zaidi wa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya
kujiimarisha.
Ninaamini hakuna timu hata moja
iliyomsajili mchezaji wa nje kwa ajili ya kupata ujiko kwamba ina wachezaji
wengi wa kigeni na inaweza kuwa na kikosi imara.
Lakini kila upande utakuwa umefanya
hivyo kwa ajili ya kujiimarisha, lengo ni kujiweka sawa kwa ajili ya mafanikio.
Mafanikio ya Ligi Kuu Bara ni mambo
mawili tu, moja ni kusaidia kupatikana kwa ubingwa au nafasi ya pili. Nafasi
hizo mbili ndiyo zinatoa wawakilishi wa Tanzania kimataifa.
Klabu zinasajili wachezaji wa kigeni
katika vikosi vya timu zao, lengo ni kufanikisha nilichokieleza hapo juu, lakini
kwa wachezaji wazawa wa timu hizo yaani Simba, Yanga na Azam wanaweza kufaidika
zaidi.
Hali halisi ilivyo, wageni wanalipwa
zaidi kuliko wenyeji. Hali hii imekuwa ikiwapoteza baadhi ya wachezaji wazawa
kutokana na kutojitambua na kisingizio ni hao wageni.
Wamekuwa na hoja za msingi kwamba hao
wageni wanalipwa kuliko wao, wapo wanaopewa nyumba na wakati mwingine usafiri,
mambo ambayo wao hawafanyiwi hata nusu yake.
Ukisikiliza wanachokisema wachezaji
wazawa kwa kweli kina hoja na klabu zinapaswa kuyafanyia kazi malalamiko yao
badala ya kuwaona sawa na wasaliti au watu wanaolalamika bila ya kuwa na hoja.
Katika kikosi, suala la usawa ni
bora lakini wachezaji nao wanapaswa kujua usawa wa kila kitu haiwezekani kwa
kuwa kila mmoja anakuwa na aina yake ya uchezaji, mchango katika timu na
tofauti hizo ndiyo maana ya timu.
Ninacholenga kuwaeleza wachezaji ni
kwamba badala ya kuwa walalamikaji, kuna kila sababu ya kuhakikisha wanatumia
makosa ya viongozi wao kuwajali zaidi kama changamoto.
Wana kila sababu ya kujiuliza maradufu
kwa nini wageni wanaonekana wako bora zaidi kuliko wao? Baada ya hapo wajifue
zaidi, wajifunze na ikiwezekana wawe na ndoto ya kupambana na kuhakikisha
wanawazidi.
Lazima tukubaliane kwamba si kweli
wachezaji wa nje ya Tanzania wanajua kila kitu kuliko wenzao wa hapa nyumbani.
Lakini kuna mambo mengi yanamsaidia mchezaji kuwa bora zaidi.
Hata mchezaji awe na kipaji cha aina
gani, lakini kama atakuwa si mwenye juhudi na anayejitambua, basi atakwama tu.
Wachezaji wa hapa nyumbani wanapaswa kujipima kama kweli wanafanya hayo mambo.
Wajiulize, ubora walionao katika
kipindi husika ndiyo mwisho wa safari na hawawezi kwenda zaidi ya hapo?
Lakini msisitizo wangu mwingine ni
hivi, anayeshindwa ni lazima ajiulize maradufu kwamba wapi aliposhindwa na baada
ya hapo apandishe kiwango chake.
Ninajua, ninaamini suala la majungu
ndani ya timu za soka kupitia wachezaji linapewa nafasi kubwa sana. Wachezaji
hamuwezi kukubali, lakini majungu katika sehemu yoyote yenye watu wengi
hayakosekani.
Wavivu wanatumia mdomo kwa mambo yao
mengi hasa unapotakiwa utendaji. Lazima wachezaji wajue ushindani ni sehemu ya
chachu ya kupandisha ubora. Sasa hawawezi kufanikiwa kushinda kwenye ushindani
kwa maneno mengi hasa kuulaumu uongozi.
Badala yake wanapaswa kuwatumia wageni
hao kama sehemu ya ushindani wa dhati na kujiimarisha. Wakiona hawana kiwango,
wanaweza kujifunza kwingine au kwa Watanzania wenzao. Katika soka kila siku mtu
anajiuliza, wapi ametoka, alipo, pia wapi anakwenda.
Kuendelea kukaa bila ya kujituma halafu
maneno ndiyo yanakuwa chachu ni kufeli tena na tena na mwisho ni kuishia
kulaumu milele bila ya mafanikio.
Mimi ninaamini vipaji au ubora wa
wachezaji wengi tu walio hapa nyumbani Tanzania. Lazima waukubali ushindani,
waingie na kupambana nao kwa njia sahihi ambazo ni kuibua na kuboresha ubora
wao ili wawe washindi. Majungu, hayajawahi kumsaidia yeyote kuwa mshindi.
0 COMMENTS:
Post a Comment