Kocha Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amesema anahitaji
wachezaji wake kucheza soka la pasi za harakaharaka wanapokuwa na mpira wakati
wanashambulia lango la timu pinzani.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki
ya kimataifa dhidi ya SC Villa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam wikiendi iliyopita na Simba
kushinda kwa bao 1-0.
Hiyo ni mechi ya sita kocha huyo kukaa kwenye benchi la Simba
tangu apewa kibarua cha kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na Ligi Kuu Bara.
Soka hilo la pasi za haraka haraka wakati timu ikiwa na mpira,
linatumiwa sana na klabu ya Barcelona ya nchini Hispania.
Kerr amesema bado kikosi chake kinahitaji marekebisho kabla ya
kuanza kwa ligi kuu, yakiwemo ya kucheza soka la kupiga pasi za haraka
wanapomiliki mpira.
Kerr alisema tatizo hilo la timu yake kutocheza soka la pasi za
haraka, ameliona kwenye mechi tano za kirafiki walizozicheza ikiwemo dhidi ya
KMKM, Polisi Zanzibar na Taifa Jang’ombe, zote za kirafiki.
“Bado wachezaji wangu hawajaushika mfumo ninaoutaka wa kucheza
soka la pasi za haraka wakati tukiwa na mpira sisi tukishambulia kwenye goli la
timu pinzani.
“Hivyo nimepanga kulifanyia kazi hilo kuhakikisha timu inacheza
soka lile ninalolihitaji ambalo ninaamini kama wachezaji wangu wakilizoea, basi
timu yangu itapata ushindi.
“Kwa mfano mechi hii dhidi ya SC Villa ya Uganda tulivyocheza
utaona wachezaji wangu walikuwa wanakaa na mpira muda mrefu bila ya kupigiana
pasi kwa wakati, hivyo ninataka kuona timu yangu inacheza soka la aina hiyo,” alisema
Kerr.
0 COMMENTS:
Post a Comment