Straika nyota wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amemuangalia beki
kisiki wa Azam FC, Muivory Coast, Pascal Wawa na kutamba kuwa lazima aipenye
safu ya ulinzi ya timu hiyo baada ya kuzisoma mbinu za wapinzani wao.
Yanga ikiwatumia washambuliaji wake Donald Ngoma, Malimi Busungu,
ilishindwa kupenya kwenye safu ya ulinzi ya Azam FC inayoongozwa na Wawa,
Aggrey Morris, Shomari Kapombe na Said Morad kufunga bao kwenye mechi ya robo
fainali ya Kombe la Kagame iliyomalizika kwa Yanga kutolewa kwa penalti 5-3.
Timu hizo zinatarajiwa kukutana kwa mara nyingine kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii itakayochezwa Agosti 22, mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Tambwe ameiambia SALEHJEMBE kuwa amegundua udhaifu wa mabeki wa
timu hiyo ambao ni wazito, hivyo hawana kasi ya kushindana na mawinga wao Simon
Msuva, Geofrey Mwashiuya, Andrey Coutinho na Deus Kaseke.
Aliongeza kuwa, hata mabao yao wanataka yatokee pembeni
wakiwatumia mawinga kwa kupiga krosi safi kabla ya kufunga baada ya kuona
katikati kugumu kupita kwenye ukuta huo.
“Kwenye mechi na Azam ile ya robo fainali ya Kagame waliyotutoa
kwa penalti, nikwambie ukweli tu kama angeanza Msuva ninaamini lazima
tungewafunga.
“Hiyo ni baada ya kuujua mfumo wao wa kujaza mabeki wengi
katikati, hivyo tumepanga kutumia mawinga tukitokea pembeni kulishambulia goli
lao na siyo katikati.
“Tumeuona udhaifu wa mabeki wao, wengi wao ni wazito, akiwemo Wawa
ambaye hana kasi ya kukimbia, hivyo tukiwatumia mawinga wetu akina Msuva na
Mwashiuya kuwambiza, ninaamini lazima tutawafunga,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment