August 24, 2015


MECHI ya Ngao ya Jamii kati ya mabingwa watetezi wa Tanzania, Yanga na waliokuwa washindi wa pili, Azam FC ilikuwa na burudani na mvuto kwa maana ya soka la ushindani.

Utaona soka lilivyokuwa likichezwa, kila upande ulionekana umepania kushinda ndani ya dakika 90 na suala la kupoteza muda lilipata asilimia chake sana.
Mwishoni kabisa wakati inaonekana kila timu ilianza kujenga hisia za kujilinda na ikiwezekana bora kwenda kwenye penalti kwa kuwa kila upande ulionekana ni mgumu.

Angalau utaona, hata ule ugonjwa wa kutokuwa na wachezaji wanaopiga mashuti kwenye Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu au minne sasa, unaonekana unaanza kupona.

Kwani upande wa Yanga walijaribu zaidi ya mara nne, hali kadhali Azam FC walifanya hivyo na kuonyesha ili ni mechi kila timu inataka kushinda.


Hisia za kwamba ushindani wa ligi sasa unahamia kwa Azam na Yanga, unaweza ukawa unajengeka kutokana na timu hizo zilivyovutana na kucheza soka la ushinda kwa asilimia kubwa sana.

Niwe wazi, ilikuwa ni mechi nzuri ambayo inaweza ikaingizwa kwenye tafsiri nyingi kupitia mpira wetu ikiwemo ile ya kama timu zitaendelea kucheza kwa kiwango hicho kwa msimu wote, dalili za mpira wa Tanzania kupanda, zitakuwa wazi.

Tofauti kubwa ambayo niliiona, wachezaji wengi walishindwa kuwa wazi au huru. Hawakujiachia na kuonyesha vipaji vyao kwa uwezo ulio sahihi au ule walionao.

Wengi walifuata mafunzo ya walimu, walihakikisha wanatekeleza kile ambacho mwalimu anataka, lakini si nyongeza kubwa kutokana na uwezo walionao au majaaliwa ya vipaji walivyonavyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Katika mechi hiyo pamoja na kuvutia kweli, bado ilionekana mechi hiyo haikuwa na mtu ambaye alikuwa ana uwezo wa kubadili mechi peke yake, iwe ni upande wa Yanga au Azam FC.

Angalau Kipre Tchetche alijaribu, mara kadhaa alijaribu kuonyesha tofauti, lakini si kwa kiwango cha kusema alikuwa “the game killer”, yaani mtu anayeweza kumaliza mchezo.
Mtu anayeweza kumaliza mchezo kwanza kabisa lazima acheze ndani ya mfumo wa mwalimu, lakini awe na ziada ambayo hata mwalimu au mashabiki hawakutegemea inaweza kutokea au anaweza kufanya.
Si lazima afunge; kuna mambo matatu anaweza kuafanya. Kwanza akawa ndiye anaanzisha mashambulizi kwa kushikilia moyo wa timu, akachezesha na kuwachanganya wapinzani huku ikionekana yeye ndiye tatizo na ameshindikana.

Anaweza kuwa ndiye hatari kwa maana ya kupiga krosi safi, anaweza kuwa mtu anayepiga vizuri mipira ‘iliyokufa’, kama timu moja wakipata afaulo basi unajua game imeisha kwa asilimia 90.

Tatu, mfungaji. Mmaliziaji bora ambaye akiingia ndani ya boksi, timu pinzani wanafumba macho kwa kuwa kusalimika kwao kunakuwa ni asilimia 10 tu.

Najua hauwezi kupinga enzi zile za kina Zamoyoni Mogella, Edibily Lunyamila, marehemu Hamis Thobias Gaga au wakongwe kama akina Sunday Manara. Swali, sasa hatuna wachezaji wa aina yao?

Ladha ya mpira haimaliziki kupitia ndani ya mfumo pekee ambao kisoka inaonekana ni ubongo wa kocha. Sasa ubongo wa mchezaji nao una nafasi yake na lazima ufanye kazi ili kutengeneza kikosi kilicho bora chenye uhakika na matokeo bora.

Kama mabingwa na washindi wa pili wanaonyesha hawana hata mchezaji mmoja anaweza kuwa na uwezo wa kubadili matokeo hasa mifumo ya makocha inapokwama, basi tatizo ni kubwa.

Bado Azam FC na mabingwa Yanga wanaweza kuwa taswira ya ligi yetu ya Bara. Hivyo ni lazima wachezaji sasa wajitambue na wacheze kwa uwezo wao walionao ikiwezekana kuuongeza kwa juhudi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic