MGOSI AKITAMBULISHWA SIMBA DAY... |
Na
Saleh Ally
SIKU
chache tu baada ya Simba kucheza mechi ya kirafiki na kuibuka na ushindi wa bao
1-0 katika Simba Day, mshambuliaji wake, Mussa Hassan Mgosi aliisaidia timu ya
Faru Jeuri kuibuka na ushindi katika michuano ya Ndondo Cup.
Mgosi
alikwenda Faru Jeuri kama timu yake ya ‘kulipwa’ ambayo amekuwa akiipa kampani
katika michuano hiyo maarufu ya Ndondo Cup.
Mgosi
aliichezea timu hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya kukabidhiwa unahodha wa
Simba, jambo ambalo niliona ulikuwa uamuzi sahihi.
Niliwahi
kueleza namna nilivyoshangazwa na uamuzi wa uongozi wa Simba kukubali Hassan
Isihaka awe nahodha wa Simba kutokana udogo wake katika soka, alishindwa hata
kujieleza.
Haikuwa
sawasawa kuona nahodha wa Mbeya City, timu changa akijieleza vizuri kabisa,
halafu nahodha wa timu kubwa na kongwe akishindwa hata kujieleza mbele ya
waandishi wa habari.
Hivyo
uamuzi wa kumpa Mgosi ambaye ninaamini kama ni miaka mingi na Simba huenda
ikawa miwili au mitatu. Ukongwe wake unaweza ukawa njia ya busara kuwasaidia
wakongwe wenzake pamoja na vijana, kuifanya Simba iende katika njia sahihi.
Lakini
niliona si sahihi kwa mara nyingine, Mgosi kuiba gharama za maandalizi ya Simba
ya kambi ya Lushoto na Zanzibar na kuitumia katika michuano ya Ndondo Cup huku
akijua si sahihi.
Pia
niliona haikuwa sawa, Mgosi kujiingiza katika hatari kubwa ya kuumia wakati
akijua maandalizi wanayofanya Simba wanategemea kumuona akiwa msaada kwenye
ligi mwezi ujao.
Tunajua
mchangani ushindani ulivyo, tunaelewa ulinzi kwa maana ya ule unaotolewa kwa
waamuzi ni tofauti angalau na ligi kuu.
Anayecheza
ndondo, haoni shida kumuumiza mchezaji fulani iwe hata kwa makusudi kwa kuwa
sidhani kama kuna kanuni kali za faini au kufungiwa.
Kama
Mgosi ataumia kwenye Ndondo Cup wakati yeye ni ‘mali’ ya Simba ambayo inamlipa
mshahara na posho zote, pia inaingia gharama kubwa kumuandaa, pia si sahihi.
Makala
haya yanaweza kuzua mjadala mkubwa, kwani wachezaji maarufu wanapokwenda kwenye
Ndondo Cup, ndiyo wanaongeza utamu wa mashindano hayo. Mimi pia kama shabiki au
mpenda soka ningependa kuona hivyo.
Lakini
unaangalia kwa maana ya maendeleo tunayoyataka kwenda katika kiwango cha
kuonekana tunafanana na soka la kulipwa, halafu hayo yanayofanyika mfano kwa
Mgosi au wenzake, tutafika huko?
Huenda
wakati wa mapumziko aliopewa na Simba angeweza kupumzika na kufanya mazoezi lakini
si kujisogeza kwenye hatari kwa kuwa mechi na mazoezi ni mambo mawili tofauti
hata kokote mtu anaweza kuumia. Si vizuri kuifanya bahati mbaya ikawa malengo!
Mgosi
ni mshikaji wangu, huenda tunaweza kuzungumza kando lakini kwa faida ya soka ya
hapa nyumbani lazima tuliweke hili wazi kwa maana ya mkongwe kama Mgosi
anapaswa kuwa wa kwanza kutambua kuwa huu kwake si wakati wa kucheza mashindano
ya mchangani nje ya Simba katika kipindi ambacho wako kwenye mapambano ya
kuifanya Simba iwe imara, irudi katika hadhi yake na yeye ni kati ya tegemeo.
Kamwe
siidharau hiyo michuano ya Ndondo Cup au mingine ya mchangani kwa kuwa pia
nimecheza sana, lakini jiulize swali hili rahisi. Kama Mgosi akiumia, unafikiri
Faru Jeuri wanaweza kuchukua gharama za kumpa matibabu sahihi? Huo mzigo
utarudi kwa Simba tena ambayo imegharimika kumuandaa.
Inawezekana
Faru Jeuri nao wanalipa vizuri, au ni mapenzi ya Mgosi kutokana na masela wake
wengi kuwa pande hizo, lakini ifikie wakati yeye aelewe, awe wazi kwao na hao
masela wamuelewe kuwa si sahihi kufanya hivyo katika kipindi hiki. Akikataa
asionekane kama anaringa, waangalie hali halisi.
Mgosi
anapaswa kuwa wazi au mkweli kwao, kama kweli anaipenda aionee huruma namna
inavyogharimika kwake na aipe heshima yake na baada ya ligi, basi huenda
atakuwa na nafasi ya kucheza michuano hiyo.
Bado
Mgosi ni kati ya washambuliaji wa kuigwa hapa nyumbani. Kama ni hivyo anapaswa
kuwa mfano uwanjani, lakini pia fikra tafakuri zake zinakuwaje hata nje ya
uwanja! Acha hoja ianze.
0 COMMENTS:
Post a Comment