Na Saleh Ally
KAMPUNI
ya simu za mikononi ya Vodacom imekubali kuingia mkataba wa miaka mitatu
mingine kuendelea kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kwa
maana ya kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri, lazima kuwashukuru Vodacom hata
kama wao pia wanafaidika kwa kiasi kikubwa. Kamwe hawawezi kusema mambo
hayaendi vizuri.
Lazima
wanapata faida ya kujitangaza kwa kuwa soka ni mchezo wenye nguvu hapa nyumbani
lakini lazima tukubali hata wangeacha kudhamini, bado wasingepata hasara.
Mkataba
wao mpya wa miaka mitatu, wameongeza hadi Sh bilioni 6.9, maana yake itakuwa ni
Sh bilioni 2.3 kila mwaka wanazotoa kwenye udhamini wao.
Hongera
tena kwa kuwa wameongeza fungu, awali ilikuwa ni Sh bilioni 4.8 sawa na Sh
bilioni 1.6 kwa mwaka. Maana yake safari hii si haba ingawa bado ninaweza
kukosoa katika mkataba huo.
Kwamba
vipengele kadhaa vimeboreshwa, lakini lile muhimu la zawadi limeachwa vile
vile. Fedha za zawadi kwa jumla zinabaki kuwa Sh milioni 174 huku tuzo za kila
mwezi zikitolewa kila mara.
Kwa
kiasi fulani wamejitutumua, lakini bado walikuwa na nafasi ya kuongeza hata Sh
milioni 50 kwenye fungu la zawadi kwa kuwa ni changamoto ya kufanya mashindano
ya ligi hiyo kuzidi kuwa juu zaidi.
Zawadi
inapozidi kuwa nono, inajenga hamasa ya juu kwa wanaoshinda, hali inayochangia
ushindani kuwa juu na watu kuwa tayari kufanya vizuri zaidi.
Wakati
yote yanafanyika, Vodacom imeamua kuwekeza zaidi katika suala la nauli za timu
ikizingatia timu mbili zimeongezeka kutoka 14 hadi 16.
Lengo
ni kuhakikisha kila timu inafika kwenye kituo kwa wakati mwafaka na kuepusha
kisingizio kingine.
Hilo
ni sehemu ya jambo zuri, lakini tunajua kwamba timu nyingi zina vyanzo vingi
vinavyoweza kuwasaidia kufika sehemu husika na fedha zilizotolewa zikabaki.
Angalia
timu zenye mabasi, zinaweza kufika vituoni kwa kutumia fedha nusu ya zile
zinazotolewa na Vodacom.
Hofu
yangu ni kwamba, baada ya Vodacom kuongeza fungu kwenye fedha hizo za nauli,
hazipaswi kuwa sherehe kwa viongozi wasio waadilifu kwa klabu zao. Najua
mtapinga lakini ukweli viongozi wengi wa klabu kubwa na ndogo ni wezi.
Wamekuwa
wakizitumia klabu kama sehemu ya kuendeshea maisha yao, ingawa wanajificha
kwenye mwamvuli wa mapenzi. Kwamba wanazipenda sana klabu hizo na wanateseka
kutokana na mapenzi yao kwa klabu zao, hakuna lolote.
Mapenzi
halafu ulale njaa, mapenzi halafu ushindwe kuhudumia familia yako. Ubaki tu
pale klabu ukiihudumia klabu, acheni kuwafanya watu hawana akili vichwani mwao.
Kama
fedha za safari zimeongezwa, basi ni wakati mwafaka hata kama zitatumika katika
kipengele kingine, basi kiwe kwa ajili ya kuboresha huduma za wachezaji wa timu
hizo za Ligi Kuu Bara.
Kama
wachezaji walikuwa kila wanapofika kambini hasa mikoani wanalala kwenye hoteli
za kubahatisha na wakakubali kwa kuwa wanajua timu haiko vizuri kifedha, basi
sasa ni wakati wa kuwaonyesha mapenzi.
Kwamba
walivumilia katika kipindi kigumu na sasa ni kipindi cha nafuu. Hivyo wanaweza
kuishi kwa hali nzuri zaidi.
Ikiwezekana
fedha hizo zinawea kutumika kama sehemu ya motisha ili wachezaji wa timu husika
wapige soka kwa moyo wa kujiamini zaidi.
Fedha
hizo zisiingie kwenye mchezo wa viongozi kuanza kufanya sherehe wakiamini sasa
ndiyo neema kwao, wachezaji waumie uwanjani mwisho fedha ziingie matumboni mwa
viongozi wajanjawajanja.
Kweli
kama viongozi, mnapambana sana lakini lazima mkubali ndiyo kazi yenu na ufahari
au mafanikio kwa kiongozi bora, pia ni kuongoza watu ambao wana amani ya mioyo
yao na kufanya kila linalowezekana kuwasaidia kufanya kazi yao vizuri.
Ongezeko
hilo la Vodacom, liwe na faida kwa wachezaji na huenda hamasa itaonekana kwa
wachezaji hali itakayosaidia mechi kuwa ngumu zaidi na kuamsha ushindani zaidi
katika Ligi Kuu Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment