Na Saleh Ally, Kartepe
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface
Mkwasa, amesema hawapo hapa kwa ajili ya kuangalia ubora wa maghorofa katika
nchi hii ya Uturuki, badala yake ni kazi kuhakikisha Nigeria wanapigwa hiyo
Septemba 5, mwaka huu.
Stars imeweka kambi kwenye mji huu wa Kartepe
nchini Uturuki kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Nigeria kuwania kucheza Afcon.
Mkwasa amesema maandalizi yanakwenda vizuri na
pamoja wamejikita vilivyo kwenye kuhakikisha ushindi unapatikana.
“Kweli, tuko makini sana kama ambavyo umeona na
tumekuwa tukijituma sana kuhakikisha kila kitu kinafanikiwa. Wachezaji wote
wako fiti kama unavyoona, kasoro Banda tu ambaye ameumia, lakini mambo
yanakwenda vizuri na kazi inafanyika,” alisema.
Jana, Stars ilifanya mazoezi mara moja tu kwa
kuwa leo ina mechi ya mazoezi dhidi ya timu ya taifa ya Libya. Awali, Stars
ilikuwa icheze mechi ya kirafiki dhidi ya Iraq, baadaye ikagundulika haikuwa
timu ya taifa badala yake ni klabu, hivyo ikaahirishwa.
Baada ya mechi ya leo, Stars haitakuwa na mechi
nyingine na Mkwasa amesema wataanza kufanya marekebisho kadhaa.
“Tutaanza kurekebisha yale ambayo tutayaona
katika hiyo mechi mazoezi. Maana tutacheza kwa lengo la kujiweka vizuri na
mechi hiyo si ya mashindano au kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa. Ndiyo maana
tutaangalia zaidi kujifunza kuliko ushindi,” alisisitiza Mkwasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment