Kiungo Mzimbabwe wa Yanga, Thabani Kamusoko ameonyesha kweli ni makini na kazi yake baada ya kwenda kuishuhudia Simba ikicheza mechi ya kirafiki.
Kamusoko ambaye ni kiungo mchezeshaji mwenye
uwezo mkubwa wa kupiga pasi za uhakika, alipewa ruhusa na klabu yake ya Yanga
kwenda kwao kuichezea timu ya taifa lakini alilazimika kubaki nchini, kisa
kikiwa ni Simba.
Kiungo huyo aliamua hivyo baada ya kusikia habari
za Simba na kuambiwa ni wapinzani wa jadi wa Yanga na ndiyo ambao wamekuwa
wakitoa upinzani mkali, hivyo baada ya kupewa ruhusa Jumapili iliyopita, akaamua
kuipotezea na kubaki Dar es Salaam ili aione Simba ikicheza katika mechi ya
kirafiki dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Taifa.
Kiungo huyo mwenye rasta, alisaini mkataba wa
miaka miwili kuichezea Yanga hivi karibuni akitokea FC Platinum ya Zimbabwe
aliyokuwa anaichezea Donald Ngoma, aliiona Simba kisha akatoa neno juu ya timu
hiyo.
Kamusoko alifika uwanjani hapo saa 9:30 alasiri
akiwa ameongozana na Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, ambapo alikaa uwanjani hapo
kwa dakika zote 90 huku akionekana kuwa makini kufuatilia kila hatua ya mchezo
huo.
“Nilipanga kurudi nyumbani kujiunga na timu ya
taifa mara baada ya mechi ya Ngao ya Jamii, lakini niliamua kubaki kuwaona
Simba mara baada ya kupata taarifa kuwa wanacheza mechi ya kirafiki.
“Sikuwa nimewahi kuwaona Simba wakiwa wanacheza,
unajua lazima niwajue wachezaji wao wenye madhara, pia aina yao ya uchezaji
wanayoitumia.
“Nimewaona na nisingependa kuzungumzia chochote
juu ya Simba ni mapema sana, lakini nikuhakikishie kuwa nitaizungumzia Simba siku
tutakayocheza nayo,” alisema Kamusoko.
Kamusoko alicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji
katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, Agosti 22, 2015 huku Haruna
Niyonzima ambaye amekuwa akicheza nafasi hiyo akianzia benchi.
Mara baada ya mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Hans
van Der Pluijm, alisifia kiwango cha mchezaji huyo ambapo alisema anaweza
kumtumia kama kiungo mkabaji pia.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Septemba 26,
2015 katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment