Straika wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe,
amezua balaa jipya katika Klabu ya Simba baada ya kocha mkuu wa timu hiyo,
Muingereza, Dylan Kerr, kuhoji kwa nini aliondoka klabuni hapo.
Kerr alifikia hatua hiyo baada ya
kumshuhudia Tambwe katika luninga akiiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa mabao
2-0 katika mchezo wake wa ufunguzi wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union ya jijini
Tanga.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani
mkubwa, uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Tambwe ndiye
aliyetoa pasi za mwisho kwa wafungaji wa mabao hayo ambao ni Simon Msuva na
Donald Ngoma.
Kiongozi
mmoja wa juu wa Simba ambaye aliomba kutotajwa jina lake, alisema Kerr baada ya
kumshuhudia Tambwe akiwatengenezea wachezaji wenzake nafasi hizo za mabao,
alihoji na kutaka kujua sababu iliyoifanya Simba iachane naye.
“Nilipomwambia sababu yenyewe alisikitika
sana kwani alidai kuwa tulimuacha mchezaji mzuri ambaye kama msimu huu
angekuwepo kikosini, basi angekuwa na msaada mkubwa sana katika kikosi chake.
“Alisema Tambwe ni mchezaji asiye na mambo
mengi uwanjani na anajua kazi yake vizuri kuwa anatakiwa afanye nini na kwa
wakati gani,” alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo, Kerr alipoulizwa kuhusiana na
jinsi alivyomuona Tambwe katika mchezo huo, alisema: “Ni mchezaji mzuri lakini
kwa sasa siwezi kumzungumzia kwa sababu hayupo kwenye kikosi changu.”
Simba iliachana na Tambwe msimu uliopita
baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri, kudaiwa kuwa ndiye
aliyependekeza afungashiwe virago vyake klabuni hapo kwa madai kuwa kiwango
chake kimeshuka.
0 COMMENTS:
Post a Comment