Straika mpya wa Azam FC, Mkenya, Allan
Wanga, ameanza Ligi Kuu Bara kwa hofu, baada ya watu kuanza minong’ono ya chini
kufuatia kiwango chake katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo juzi Jumamosi
wakati Azam ikichomoza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons.
Katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye
Uwanja wa Azam Complex, Wanga ambaye amejiunga na Azam akitokea Al-Merrikh ya
Sudan, alikosa nafasi nyingi za wazi kabla ya kutolewa na nafasi yake
kuchukuliwa na Ame Ali ‘Zungu’ kipindi cha pili.
Hata hivyo, mchezaji bora wa Kagame, Pascal
Wawa, ameonya na kusema pengine mashabiki hawamjui kuliko yeye ambaye amefanya
naye kazi kwa misimu miwili kule Sudan kabla ya kuungana tena Chamazi.
“Kwangu mimi ni furaha kubwa sana kucheza na
Allan. Miongoni mwa washambuliaji mahiri, basi yumo kwenye orodha yao. Ninamjua
pengine kuliko mwingine hapa Tanzania, nimecheza naye Al-Merrikh kwa misimu
miwili lakini kidogo tulipishana kikazi, lakini sasa tunaungana kupiga kazi.
“Siwezi kumsemea uzuri wake, jicho la kila
mmoja litajionea kazi yake,” alisema huku akiachia tabasamu kubwa.
Katika mchezo huo, Wanga alikosa mabao ya
wazi matatu huku mojawapo akigongesha mwamba wa juu kipindi cha kwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment