Baada ya straika wa Simba, Mganda, Hamis Kiiza, kuanza ligi kwa
kufunga bao moja, kocha mkuu wa kikosi hicho, Muingereza, Dylan Kerr, ameibuka
na kusema anahitaji kumuona straika huyo akifunga zaidi ya mabao 20, msimu huu.
Awali, wakati Kiiza anatua Simba na kupewa mkataba wa miaka
miwili, mashabiki wa soka walikuwa wakisikika wakisema kuwa straika huyo hawezi
kutatua tatizo la ufungaji klabuni hapo jambo ambalo Kerr alilipuuzia.
Hata hivyo, licha ya Simba kusajili mastraika kadhaa, lakini
iliendelea kuhangaika huku na kule kutafuta straika mwingine wa maana ambapo
iliwaleta nchini baadhi ya wachezaji kufanya majaribio, lakini mwisho wa siku
ikaamua kumchukua Msenegali, Pape Abdoulaye Nd’aw.
Kikosi cha Simba, kwa sasa kina washambuliaji watano ambao ni
Mussa Hassan Mgosi, Danny Lyanga, Ibrahim Ajib, Kiiza na Nd’aw.
Hata hivyo, kocha huyo mwenye uwezo wa hali ya juu, amesema kuwa
amempa Kiiza kazi maalum ya kuhakikisha anafunga mabao 20 tu kwenye ligi msimu
huu.
“Nimefurahi kumuona Kiiza akianza kwa kufunga, kitu ambacho
nilikuwa nasubiria kukiona kutokana na watu kumsema vibaya na kuninukuu mimi
vitu ambavyo sijaongea, sasa naamini hawataweza tena kuongea vibaya juu yake.
“Pia nataka kuona mastraika wangu kila mmoja akifikisha zaidi ya
mabao kumi msimu huu, lakini itakuwa vizuri zaidi kama Kiiza akifikisha mabao
20, hili ni jukumu lake,” alisema Kerr.
0 COMMENTS:
Post a Comment