Na
Saleh Ally
KESHO
ndiyo ile siku kila mpenda soka nchini alikuwa akiisubiri kwa hamu pale kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wapo
watakaokaa kimya nyumbani wakitaka kuiona mechi hiyo moja kwa moja kupitia
runinga ya Azam TV ambayo huonyesha mechi za Ligi Kuu Bara.
Lakini
wapo ambao hawatakubali, watahakikisha wanafika Uwanja wa Taifa ili waishuhudie
wakiwa pale uwanjani. Hao ni wale wenye nafasi ya kufanya hivyo.
Mechi
ya Simba ambao watakuwa wenyeji wa watani wao, Yanga, itakuwa na mvuto sana na
inawezekana ikashuhudiwa na watu wengi zaidi kuliko mara nyingine kutokana na
mvuto huo.
Ushindi
wa kila timu katika mechi tatu za mwanzo za Ligi Kuu Bara ndiyo umeongeza mvuto
zaidi wa mechi hiyo ya kesho.
Kwa
maana ya takwimu kupitia mechi tatu ambazo kila timu imeishacheza, jibu
linaonekana kuwa hivi, itakuwa ni mechi ya ushindani wa juu na matokeo ambayo
si rahisi kubashiri kirahisi.
Ukiangalia
uwezo wa Simba na Yanga kwa maana ya uwanjani, hauna tofauti kubwa sana. Yanga
wamefunga mabao 9, Simba wamefunga 6 na kila timu imefungwa bao moja tu.
Zote
mbili zilianza kushinda na mabao ya idadi ndogo, halafu zikaenda zinaongeza
idadi ya mabao ya kufunga. Simba ilianza na bao moja, hadi mechi ya tatu
ikashinda mabao 3-1. Yanga ilianza na ushindi wa mabao mawili, hadi mechi ya
tatu ikawa imeshinda mabao 4-1.
Kwa
takwimu hizo, ni hatari sana kwa shabiki yeyote kwenda uwanjani akiwa na
matokeo yake kichwani, kwenda na matokeo mfukoni, haitakuwa sahihi.
Simba
vs Yanga, Uwanja wa Taifa, kesho ni mechi ambayo timu yoyote inaweza kushinda,
timu yoyote inaweza kupoteza na pia kuna uwezekano wa sare.
Kwa
yeyote anayekwenda uwanjani, anatakiwa kwenda kiuanamichezo zaidi. Akili yake
aielekeze kwenye hili; kwamba ni mchezo wa soka ambao timu yoyote inaweza
kushinda, kupoteza au kukatokea ahueni ya sare.
Mara
kadhaa, tumeona mashabiki wanazimia pale uwanjani na hii inatokana na mashabiki
wengi kwenda uwanjani wakiamini timu fulani ndiyo yenye uwezo mkubwa wa
kushinda kuliko nyingine, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.
Mfano,
mashabiki wa Simba, wamekuwa wakiamini Yanga ni wepesi sana kwao. Bado
wanapaswa kujua Yanga ya sasa ina mabadiliko makubwa na ina wachezaji wanaoweza
kubadilisha yale yaliyozoeleka hapo awali.
Kuna
la kukumbuka kuhusiana na mchezaji mmojammoja ambao Yanga na Simba wanao.
Kwamba ni wachezaji wanaoweza kubadili matokeo kwa kupitia uwezo au vipaji
vyao.
Wachezaji
ambao wakati mwingine bila ya mfumo wa kocha, wanaweza kufanya mambo tofauti
kabisa na kushangaza.
Nitakukumbusha,
mechi ya mwisho ambayo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga,
utaona lile bao alilofunga Emmanuel Okwi.
Bao
la Okwi halikuwa la mfumo tena, badala yake kipaji na uwezo mkubwa au kipaji
cha juu cha mchezaji, ndicho kilichoamua matokeo ya mechi ile.
Maana
yake, Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima kwa upande wa
Yanga, Hamis Kiiza, Said Ndemla, Ibrahim Ajibu, Mussa Hassan Mgosi na wengine,
pia wanaweza kuamua matokeo ya kesho.
Sasa
kwa wale wanaokwenda uwanjani, ili kuepusha ghadhabu zisizokuwa na msingi au
kuepusha watu kuzimia au kupata matatizo, lazima wajue ni mechi ambayo matokeo
yanaweza kuwa mabaya au mazuri kwa upande wowote.
Simba
na Yanga, kesho, hata kama unaangalia kwenye runinga, basi hakikisha kwamba
matokeo yatapatikana baada ya dakika 90, yale ya kichwani mwako au mfukoni,
achana nayo, yatakuumiza.
0 COMMENTS:
Post a Comment