September 25, 2015


KOCHA MSAIZIDI WA YANGA, CHARLES BONIFACE MKWASA.

Na Saleh Ally
GUMZO la mchezo wa kesho halizuiliki, ndiyo maana tumekuwa tukiwaomba hata Wanasiasa na kampeni zao, kuendelea lakini wajue wenye nchi sasa wanakaribia kukutana, hivyo hakuna wa kulizuia hilo.


Hata kama utakwenda kwenye sehemu zina kampeni ya mambo ya siasa, bado mechi ya kesho ya watani Yanga na Simba, ndiyo gumzo.

Simba na Yanga zinakutana huku kila upande ukitamba kuwa una uwezo. Gumzo la kishabiki ni hili; Yanga wanasema wako vizuri, lakini Simba hawahitaji hata takwimu kwa kuwa wanajua Yanga ni ‘wao’, watachukua pointi zao mapemaa.

Soka haliko hivyo ingawa hesabu za nyuma zinaweza kutumika kuangalia mchezo unaweza kuwa vipi. Bado hilo halizuii watakaoushuhudia mchezo huo, kulazimika kusubiri dakika 90 ziishe kwa kuwa ndiyo jibu sahihi.
 
KOCHA MSAIDIZI WA SIMBA, SELEMANI MATOLA.
Katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara kwa kila kikosi, zinaonyesha Yanga na Simba, zote zina vikosi imara hali inayozidisha ugumu wa mechi hiyo.
Kila timu imeshinda mechi zote tatu, tofauti ni ndogo sana ingawa kitu kimoja zimelingana kwani zilienda zinaongeza idadi ya mabao ya kufunga katika kila mechi.

Simba ambao ni wenyeji kesho, walianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Sports, wakaongeza 2-0 dhidi ya Mgambo kabla ya kuipiga 3-1 Kagera Sugar.

Yanga waliwachapa 2-0 Coastal, wakapandisha idadi kwa kuitandika 3-0 Prisons kabla ya kukutana na JKT na kupiga 4-1.

Baada ya hapo, utaona Yanga imefungwa bao moja huku Simba ikiwa imefungwa bao moja pia, lakini goal difference (tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa) Yanga wanayo kubwa licha ya kufungwa bao moja. Yanga wana 9 na Simba wana 6.

Simba na Yanga zote zinaingia uwanjani zikiwa na vikosi bora, ingawa hiyo haizuii jibu la ushindi kwa timu nyingine.

Ukitaka uangalie katika upachikaji wa mabao, katika mabao 6 iliyofunga kwenye mechi tatu, Simba imefunga mabao yake mawili katika kipindi cha kwanza na manne kipindi cha pili.

Yanga imefunga mabao tisa, kati ya hayo, matano katika kipindi cha kwanza na manne kipindi cha pili.
Hapa utaona zinakutaka timu zenye uwezo wa kufunga wakati wowote ingawa kwa Simba inaonekana asilimia 75 ya mabao yake ni kipindi pili. Maana yake unapoingia nao kipindi cha pili haujawafunga, basi ujue una hatari kubwa ya kupoteza.

Katika kipindi cha pili wamefunga mabao yao katika dakika za 46, 56, 73 na 90. Inaonyesha kuanzia mwanzo hadi mwisho kinaweza kuwa kipindi chao kwa kuwa wana uwezo wa kufunga wakati wowote.

Mabao mawili ya Simba katika kipindi cha kwanza ni dakika za 27 na 31, hii nayo inaonyesha Simba si wazuri sana dakika za mwanzo kwa kuwa chini ya dakika 20 hawajawa na bao, wanapanda kasi taratibu sana.

Yanga wanaonekana si rahisi kuwabashiri, kwani katika mabao yao, matano ya kipindi cha kwanza wamefunga mapema hadi mwishoni. Wamefunga katika dakika za 8, 27, 30, 42 na 44 na kisha dakika za 42, 62, 66 na 87.

Utaona ufungaji wao ni ule uliogawanyika, ule ambao haujui utafanyika katika kipindi gani na hii ni sehemu ya kuonyesha ni kikosi kinachotafuta mabao kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

Unaweza kusema Yanga ni hatari sana mwanzoni, katikati na mwishoni wakati Simba wanaonekana kuwa ni wakali kuanzia dakika za katikati mwa kipindi cha kwanza hadi mwishoni.

Kitakwimu mechi ni ngumu sana, pia haionyeshi kama kuna timu bora sana kwa kiwango cha juu kuliko nyingine.

Simba:
Mabao
Imefunga 6
Imefungwa 1

Kipindi cha kwanza:
Bao 2

Kipindi cha Pili:
Bao 4


Yanga:
Mabao
Imefunga 9
Imefungwa 1

Kipindi cha kwanza:
Bao 5

Kipindi cha Pili:

Bao 4

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic