September 25, 2015


Muda mfupi kabla ya Yanga kuivaa Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amezua hofu katika kambi ya timu hiyo baada ya kuumia na kulazimika kukaa nje ya uwanja katika mazoezi ya timu hiyo.


Cannavaro alikutwa na majanga hayo juzi katika Uwanja wa Gombani, yalikofanyika mazoezi ya Yanga. Timu hiyo imeweka kambi kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba.

Mazoezi ya Yanga yalianza saa 10:00 jioni na kumalizika saa 12:18 jioni huku yakihudhuriwa na mashabiki wengi, lakini Cannavaro ambaye alianza mazoezi pamoja na wenzake, ghafla alianza kulalamika maumivu ya kifundo cha mguu.
 
PICHA YA MAKTABA. CANNAVARO AKITIBIWA BAADA YA KUUMIA MAZOEZINI, HII NI MWEZI MMOJA ULIOPITA KWENYE UWANJA WA TAIFA.
Hali hiyo ilisababisha Daktari wa Yanga, Juma Sufiani, kuanza kumpatia huduma ya kwanza, ambapo alimfunga mabarafu katika sehemu aliyoumia, beki huyo aliendelea kukaa nje ya uwanja mpaka mazoezi yalipomalizika.

Yanga haikufanya mazoezi jana asubuhi, badala yake ilitarajiwa kufanya mazoezi jana jioni kwenye uwanja huohuo kabla ya kurejea leo Ijumaa jijini Dar.


Sufiani hakupatikana kuzungumzia juu ya majeraha hayo wakati Cannavaro naye alipigiwa simu lakini hakupokea. Tangu Yanga itue kisiwani hapa, kumekuwa na ulinzi mkali na ni vigumu kuwafikia wachezaji au watu wa benchi la ufundi la timu hiyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic