Na Saleh Ally
UTURUKI ni moja ya nchi zenye historia
ya kuvutia katika soka duniani na kama unaitaja, klabu mbili kubwa za
Galatasaray na Fenerbahce ndizo nembo kutokana na ukongwe na ubora wake.
Kuna timu nyingine kama Besiktas na
Antalya Spor lakini haziwezi kuwa na rekodi au historia ndefu kama timu hizo
mbili kongwe.
Galatasaray ndiyo kongwe zaidi,
ilianzishwa Oktoba 30, 1905, bado siku chache ikamilishe miaka 110. Fenerbahce
ilianzishwa mwaka 1907, ina umri wa miaka 108.
Klabu hizo ni kongwe, nimeanza kutaja
umri kuonyesha kweli ni kongwe na tunaweza kujifunza kupitia zenyewe.
Ndiyo maana nilipokuwa nchini Uturuki
nilifanya juu chini kuhakikisha ninafanya ziara katika makao makuu ya klabu
zote mbili, pia nikatembelea viwanja vyao vya nyumbani.
Galatasaray inatumia Uwanja wa Turk
Telecom Arena wenye uwezo wa kubeba watu 52,652 na Fenerbahce nyumbani ni
kwenye Uwanja wa Sukru Saracoglu unaochukua watu 53,715 walioketi.
Saracoglu ni jina la moja wa viongozi
wake mashujaa waliowahi kuiongoza klabu hiyo na kuleta mapinduzi makubwa ya
kimaendeleo akiwa madarakani kwa miaka 16, pia alikuwa mmoja wa mawaziri wa
serikali ya Uturuki.
Wakati nikiwa katika ziara ya makao
makuu ya klabu hizo niligundua mambo mengi sana ya kujifunza. Huenda baadhi
nitarudia kama nilivyofanya wakati nilipotembelea viwanja na makao makuu ya
klabu za Ujerumani za Bayern Munich na Borussia Dortmund.
Nikiwa pale, niliwakumbuka Yanga na
Simba, klabu kongwe za Tanzania ambazo hazina viongozi wabunifu hata kidogo.
Viongozi ambao wanafanya kama
walivyofanya viongozi wa miaka kibao nyuma. Ni kusajili na kuiandalia timu
kambi, baada ya hapo ni ligi, kazi imeisha. Wanachosubiri ni ushindi
washerekee, au wapoteze walaumiane.
Fenerbahce:
Uwanja na ofisi zao ziko upande wa Bara
la Asia ingawa ni katika Jiji moja la Istanbul.
Uturuki ni nchi moja iliyo katika mabara
mawili ya Asia na Ulaya, vivyo hivyo Jiji la Istanbul ambalo lina watu milioni
14 kwa mujibu wa sensa ya Desemba 2014.
Unapofika kwenye Uwanja wa Sukru Saracoglu,
mandhari ni bora na kwa kuwa niliwasili pale saa 4 asubuhi, Robin van Persie,
Nani, Diego na wengine walikuwa mazoezini. Ulinzi ni wa kutosha katika eneo
hilo.
Baada ya matembezi ya sehemu mbalimbali,
niligundua mambo mengi mfano kumbukumbu za kutosha za klabu huyo.
Kwenye nyumba ya makumbusho kuna
makombe, jezi za zamani zilizochezewa mechi. Jezi za mashujaa wao.
Kuna vikombe zaidi ya 160 ambavyo timu
hiyo ilicheza na kuvibeba katika michuano mbalimbali ya Ulaya na ndani ya nchi
hiyo. Ngao za Jamii pia medali.
Pamoja na makombe, wamekumbuka kuweka
sanamu kadhaa, mfano sanamu tatu zinazowaonyesha watu wakifanya kikao. Hicho
ndiyo kilikuwa kikao cha kwanza kilichoizaa klabu hiyo.
Picha za viongozi wa klabu hiyo, kuanzia
mwaka 1907 hadi sasa. Huku zikiwa zimetengenezewa sehemu maalum ya viongozi.
Ukitoka hatua chache kidogo
unaingia kwenye duka ambalo linauza vifaa mbalimbali kama jezi, fulana, mabegi,
makoti, saa na bidhaa nyingine mbalimbali.
Hata kukiwa hakuna mechi, Fenerbahce
imeajiri wafanyakazi 107 kama utazungumzia madereva, wafagizi, wahasibu,
watendaji na wengine wengi.
Duka lake la vifaa huweza kuingiza hadi
dola 2,100 (Sh milioni 4) kwa siku au zaidi kama si siku ya mechi. Katika siku
ya mechi, huingiza hadi dola 15,000 (Sh milioni 30) kwa siku.
Galatasaray:
Huenda hii ni maarufu zaidi kwa hapa
nyumbani Tanzania na imekuwa nembo ya Uturuki hasa ukizungumzia soka la nchi
hiyo. Uwanja wake upo Istanbul pia lakini upande wa Bara la Ulaya.
Hakuna tofauti yoyote na Fenerbahce
kutokana na hifadhi kubwa ya makombe pamoja na kuonyesha thamani kwa watu
waliotoa mchango kwa maendeleo au uanzishwaji wa klabu hiyo.
Pia kuna duka lililopo klabuni. Lao
linaonekana kuwa kubwa zaidi ya lile la wapizani wao ingawa kimapato
wanaonekana hawana tofauti kubwa hata kidogo ila uwanja wake unaingiza watu
wengi.
Duka la Galatasaray ni kubwa zaidi na
ndani yake kunapatikana kila aina ya jezi na fulana za timu hiyo inayotumia
rangi ya njano na damu ya mzee.
Pamoja na fulana na jezi, utaona kuna
saa za mkononi na ukutani, vikombe, ‘makava’ ya simu na vibeba ufunguo.
Ami Sukru ambaye ni mmoja wa wasimamizi
wa masuala ya waandishi na ulinzi pia katika klabu hiyo, anasema vitu kama
vikombe, vibeba ufunguo, saa za ukutani, mezani na mkononi ndiyo zinazoingiza
fedha nyingi zaidi.
Anaamini kwa mwezi klabu hiyo huingiza
hadi dola 100,000 (zaidi ya Sh milioni 210) baada ya mauzo katika maduka
mbalimbali ya Jiji la Istanbul.
Kawaida unapokwenda katika maduka
makubwa mfano wa Mlimani City na Quality Centre, unakutana na maduka ya klabu
hizo pia. Watu mbalimbali wenyeji na wageni wanaingia kupata huduma.
Mpangilio mzuri, utaona karibu kila
sehemu yamegawanywa mara tatu. Sehemu ya wanaume, wanawake na watoto na wote
wanapata bidhaa zao zikiwa katika nembo za klabu hiyo.
Biashara ni mtaji; Yanga na Simba wana
mtaji mkubwa hata kama utakuwa si sawa na ule wa Galatasaray na Fenerbahce. Wanauza
nini? Jezi zimewashinda, fulana hawawezi! Nguo za watoto hawajui. Je, hata
vikombe, saa na vibeba ufunguo vinawashinda?
Kila anayeanzisha bishara anajiuliza
mtaji atapataje na atauza wapi. Simba na Yanga zina uhakika wa kupata mtaji,
hata zikikopa zina uhakika wa kurudisha kwa kuwa wanunuzi ambao ndiyo mtaji
mkubwa au uhakika wa biashara wapo. Sasa mbona wanalala tu!
0 COMMENTS:
Post a Comment