Na Saleh Ally
MWISHONI mwa Machi, mwaka huu Barcelona
ilifanikiwa kuibuka na ushindi kwa kuifunga Real Madrid kwa mabao 2-1 ikiwa
inacheza nyumbani Camp Nou jijini Barcelona.
Ushindi wa Barcelona ulikuwa muhimu sana
ili kuiacha Madrid kwenye uhakika wa kubeba ubingwa.
Mechi hiyo ya El Clasico ilikuwa ni ya
kuua ndege wawili kwa jiwe moja, kuifunga Madrid ghali pia kujiweka katika
nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Shukrani ya mabao ya beki Jeremy Mathieu
na Luis Suarez. Barcelona ikaibuka na ushindi huo muhimu sana.
Kabla ya mechi na hata ilipoanza,
mashabiki wa Barcelona walibeba vipeperushi vilivyokuwa vikionyesha namba 12,
huenda wengi hawakujua ni kwa nini.
Mashabiki zaidi ya 95,000 wa Barcelona
waliweka rekodi ya kupiga kelele kwa nguvu kuliko wakati mwingine wowote wa
mechi za La Liga huku wakiishangilia timu yao kwa nguvu za ajabu na kuwazomea
Madrid, hali iliyoelezwa kuchangia kuwavuruga Cristiano Ronaldo na Gareth Bale
waliokuwa tegemeo la Madrid siku hiyo.
Leo Watanzania wanashuka uwanjani wakiwa
na kazi moja tu kubwa, ‘kucheza’ na kuisaidia Taifa Stars kushinda mechi
ngumu dhidi ya Nigeria ‘Super Eagles’ ikiwa ni kuwania kucheza Kombe la Mataifa
Afrika.
Mashabiki wa Tanzania wanaiweza kazi ya
kuwa mchezaji wa 12 uwanjani. Ndicho walichokuwa wakimaanisha mashabiki wa
Barcelona siku ile kwamba wao wanaifanya Barcelona icheze na mtu mmoja zaidi
uwanjani kwa kuwa wanawapa wachezaji wao nguvu ya kufanya vizuri huku
wakiwavuruga Madrid na kuwasababisha wacheze utafikiri wapo pungufu.
Swali, mimi, wewe na wengine tunaweza
kucheza nafasi ya mchezaji wa 12 uwanjani na kuisaidia Taifa Stars kuibuka na
ushindi kesho?
Jibu ni ndiyo ingawa kuna mawili kwa
kila atakayekwenda uwanjani anaweza kuchagua, kucheza namba 12 upande wa Taifa
Stars au Super Eagles.
Kwani kama utakwenda uwanjani na kukaa
kimya tu au kuizomea Taifa Stars eti kwa kuwa wachezaji wamekosea, basi utakuwa
unaishambulia Taifa Stars na huenda ukawa upande wa Nigeria bila ya kujua.
Kikubwa ambacho wanapaswa kukumbuka
mashabiki wote wanaokwenda Uwanja wa Taifa kutakapochezwa mechi hiyo ni kwamba
wachezaji wa Taifa Stars lazima watakosea kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa.
Ikitokea wamekosea, kushangaa si vibaya.
Lakini ni muhimu sana kuwapa moyo na kuwaonyesha mpo nao kwa dakika zote 90.
Kwa haki, lazima tukubali Nigeria
wamepiga hatua kisoka kuliko sisi. Wana fedha kuliko sisi lakini hawawezi kuwa
na mioyo imara na yenye nguvu ya ushindi kuliko Watanzania wote watakaokuwa
uwanjani leo.
Taifa Stars ni timu yangu, yako wewe na
Watanzania wengine. Huenda hukuwahi kupata nafasi ya kuwa mzalendo, leo nafasi
unayo kubwa na hasa ukijua Taifa Stars inapambana na timu kubwa katika soka la
Afrika.
Hakuna kisichowezekana, Taifa
Stars kutafuta ushindi na kufanikiwa dhidi ya timu kigogo kama Nigeria na
kufanikiwa kushinda haiwezi kuwa mara ya kwanza.
Wanaoweza kuunganisha nguvu ya
kuhakikisha mchezaji namba 12 anacheza kwa kiwango kizuri ni Watanzania
wenyewe.
Kutoka uwanjani tumefungwa kutatuumiza
sana. Kutoka tukiwa na ushindi, itakuwa ni sherehe yenye furaha isiyokuwa na
mfano.
Haya yote yapo ndani ya mikono ya
Watanzania. Kikubwa ni kuamini, mchezo wa soka hauwezi kuchezwa bila ya makosa
na lazima mambo yaharibike na kurekebishwa hadi ushindi utakapopatikana.
Hivyo tusiende uwanjani na kuwaachia
Taifa Stars wachezaji kama kikosi kilicho ugenini sawa na Nigeria walio
ugenini.
0 COMMENTS:
Post a Comment