Na
Saleh Ally, aliyekuwa Istanbul
WAKATI
wa Kombe la Dunia mwaka 1994, timu ya taifa ya Romania ndiyo ilikuwa gumzo
zaidi licha ya kwamba Brazil ikiongozwa na Romario na Bebeto ndiyo ilifanikiwa
kubeba ubingwa.
Pamoja
na Bebeto na Romario ilikuwa vigumu kutowazungumzia wachezaji wawili, beki wa
Marekani, Alex Lalas, jamaa aliyekuwa na mzuzu mrefu. Halafu Gheorghe Hagi
aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Romania.
Hagi
alifunga mabao matatu katika michuano hiyo, moja likiwa ni dhidi ya Argentina
na jingine dhidi ya Colombia ambalo lilikuwa moja ya mabao bora ya michuano
hiyo.
Alifunga
umbali wa mita 40 baada ya kugeuka na kuachia mkwaju iliomshinda kipa Oscar
Cordoba. Mwisho wa michuano hiyo licha ya kuishia robo fainali, Romania
ikachaguliwa kuwa timu bora ya michuano.
Kwao
Romania, Hagi anajulikana kama Regele, yaani mfalme. Jina ambalo anastahili,
kwani licha ya kuingoza timu ya taifa kwa mechi 124 na kufanikiwa kufunga mabao
35, aliipa nchi hiyo heshima kubwa akichezea timu kubwa duniani kama Barcelona
na Real Madrid.
Hagi
alimalizia soka lake Galatasaray ya Uturuki, alianza kuichezea kuanzia 1996
hadi 2001 alipostaafu soka.
Baadaye
akapata nafasi ya kuifundisha msimu mmoja na akaiwezesha kubeba ubingwa huku
ikiwachapa wapinzani wake wakubwa Fenerbahce kwa mabao 5-1 hiyo ilikuwa mwaka
2004 hadi 2005.
Baadaye
alitimuliwa, halafu akarejea na kuifundisha timu hiyo tena kuanzia mwaka 2010
hadi 2011, akatimuliwa tena kutokana na kutofanya vizuri.
Sasa
Hagi ni shujaa wa Galatasaray na heshima yake imeendelea kubaki juu kwa kuwa
akiwa mchezaji aliisaidia kubeba makombe ya ligi na michuano mingine.
Siku
tano zilizopita nilikuwa katika makao makuu ya klabu ya Galatasaray jijini
Istanbul ambako nilifanya ziara fupi ya kujifunza mambo.
Mengi
nimeshangaa, mengi nimejifunza lakini kwanza nianze na lile la kuona jezi namba
10, tena katika mfumo wa jezi za sasa za Galatasaray ikiuzwa kwa bei juu
kabisa.
Fedha
ya Uturuki inajulikana kwa jina la Lira, hivyo jezi moja yenye jina namba ya
Hagi ni Lira 241. Ukibadilisha dola 100, unapata Lira 261 hadi 280.
Utaona
jezi hiyo ina thamani kubwa, takribani dola 10 ya Marekani. Bei hiyo ni sawa na
zile za nyota wengine wa sasa wa Galatasaray kama Wesley Snejdeir na Karel Podolski!
kwangu kilikuwa kitu kigeni, nikajifunza kwa kuuliza.
Aliyeniongoza
katika ziara hiyo ya mafunzo, kanieleza inatokana na heshima kubwa ya Hagi
akiwa kocha na mchezaji. Wanaitambua na kuithamini hadi leo.
Tena
akanieleza, jezi hiyo imekuwa ikiingiza fedha nyingi kimauza na Hagi naye
amekuwa akifaidika!.
Haraka
nikakumbuka wachezaji wa zamani wa Yanga na Simba kama Makumbi Juma au enzi
zile za kina Abdallah Kibadeni.
Nikaona
labda ni mbali sana, vipi sasa akina Edibily Lunyamila au hivi karibuni watu
kama Juma Kaseja na Selemani Matola. Hawa si walizipa Yanga na Simba makombe?
Hawa si walizipa timu zao heshima?
Mbona
Yanga na Simba hawataki kufanya biashara wala hawataki kuwa wabunifu. Au
viongozi wana hofu leo wakiuza jezi za kina Lunyamila na Kaseja watafunikwa
umaarufu wao?
Yanga
na Simba si wabunifu wa biashara kwa kuwa hawafikirii mbali? Hawana watu enye
uwezo mkubwa wa kufikiria au zaidi wanawaza leo tu, hakuna anayejua klabu hizo
zitafika kesho?
Maswali
ni mengi, wanaoweza kuyajibu ni Yanga na Simba wenyewe ingawa najua longolongo
na sababu lundo zisizo na msingi zitatawala lakini habari ndiyo hiyo. Hadi leo
Galatasaray wanauza jezi ya Hagi. Yule shujaa wa Romania mwaka 1994 na shujaa
wao hadi mwka 2001. Jifunzeni na mkubali na muacha kupokea mambo yakapita sikio
moja na kutokea jingine halafu mkaendelea kubaki vilevile!
0 COMMENTS:
Post a Comment