Na Saleh Ally
ADHABU kali zaidi katika maisha ya
mwanadamu kama anakosea ni ile ya kifo au kifungo cha maisha jela. Kwa kauli
nzuri, adhabu hizo ni kumaliza maisha na uhuru wa mwanadamu.
Hakuna ambaye angependa akumbane na
balaa la moja ya adhabu hizo ingawa hakuna anayeweza kukataa kwamba binadamu
wameumbwa na makosa.
Kila mmoja anakosea katika maisha
ya kila siku, lakini anayepunguza makosa maana yake anaongeza umakini na ndiyo
unaweza kumuita ni mtu makini.
Mwanafilosofia, Benjamin Spock,
anasema: “Trust yourself. You know more than you think you do.” (Jiamini,
unajua zaidi ya yale unayofanya).
Kukosea kunatokea kwa binadamu
yeyote, lakini ukijiamini na kuyatumia makosa yako kujifunza, unakuwa na
uhakika wa kufanya bora zaidi.
Kipa Juma Kaseja amerejea uwanjani
kwa mara nyingine akiwa na Mbeya City. Kikosi cha Mbeya City kimekuwa shujaa
kwa mambo mawili, kwanza utambuzi na pili uamuzi sahihi.
Mbeya City wameng’amua Kaseja bado
ni mmoja wa makipa bora nchini, mwalimu au kaka wa makipa wengi sana, hivyo
uwezo wake bado utakuwa msaada kwao.
Lakini Mbeya City imeonyesha
inaweza kufanya maamuzi ambayo yanajitegemea kwa kumsajili Kaseja. Ingawa ni
muda mfupi, miezi sita tu. Itakuwa ni nafasi kwake Kaseja kujipima na kuonyesha
kweli anaweza.
Mwanafilosofia mwingine aitwaye Eckhart
Tolle alipenda kutumia msemo huu: “The past has no power over the present
moment.” (Yaliyopita hayana nguvu kwa wakati uliopo)
Hii ndiyo anatakiwa kuitumia
Kaseja na kurejesha uwezo wake. Kufanya kazi yake kwa uhakika, jambo ambalo
limeanza kuonekana katika mechi mbili za Mbeya City.
Wakati Kaseja anaanza kuonyesha kweli
uwezo anao, wakati anaanza kuonyesha kweli amepania kuitumikia Mbeya City
ambaye ni mwajiri wake, tayari chokochoko zimeanza kutoka upande mwingine.
Itakuwa rahisi wengi kulikataa hili,
lakini kuna uhakika wa asilimia zote kwamba kuna baadhi ya viongozi ambao
wanatokea katika moja ya timu ambazo Kaseja alizichezea, walianzisha maneno kwa
kuwapigia viongozi wa Mbeya City kuwaeleza yaliyopita ya kipa huyo.
Walikuwa wakilalama kuwa Kaseja
alikuwa tatizo, aliwafungisha na vinginevyo. Kitu ambacho unaweza kukiita ni
cha kipuuzi, cha kushangaza na sehemu ya kuonyesha kiasi gani wako viongozi
ambao walistahili kuitwa wanaubabaisha mpira wa Tanzania, ndiyo maana haukui.
Kama kiongozi aliamua kuachana na
Kaseja, unakumbuka alikuwa Simba, akaenda Yanga nao wakamuacha akakubali kukaa
nje ya uwanja msimu na ushee.
Sasa amepata kazi Mbeya City,
baadhi ya viongozi wameanza kuzungumza na watu wa City wakiwaambia kwamba kipa
huyo hafai kabisa, tena hata kidogo.
Mbeya City ni watu wazima, wana akili
timamu, wanaweza kung’amua na kuamua mambo yao, ndiyo maana wapo hapo walipo,
sasa kuna haja gani ya kuwaeleza kuhusiana na mchezaji fulani suala la ubora
wake?
Inawezekana ni hofu ya viongozi
waliosema Kaseja hana msaada hata kidogo, waliona ni bora aendelee kukaa nje
ili asicheze. Wana hofu akicheza na kufanya vizuri, basi wataonekana walikosea.
Kaseja atabaki kuwa kipa bora, ana
nafasi ya kubaki juu au kupungua kwa ubora kama mwenyewe ataamua. Huenda huu
ndiyo wakati wa yeye kuzidisha utulivu maradufu ya ule na kuitumikia Mbeya City
kwa juhudi kuu na kuiletea mafanikio.
Viongozi wa klabu moja wanaopoteza
muda kwenda kwenye klabu nyingine kuzungumza maneno ya umbeya ni jambo la
kusikitisha sana. Wanaonyesha kiasi gani wana chuki, wanaonyesha kiasi gani
hawana uwezo wa kusaidia maendeleo na badala yake chuki na visasi ndiyo vimejaa
kwenye mioyo na vichwa vyao.
Aina ya watu hawa, unafikiri lini
watakuwa na muda kwa ajili ya maendeleo ya mpira? Mtu waliachana naye bado
wanaendelea kumtakia mabaya, mtu ambaye anapambana na maisha kwa juhudi zake
binafsi.
Si sahihi kumhukumu Kaseja iwe ni
kifungo cha maisha au kuchukua shingo yake. Wamwache ajitafutie, wamwache
apambane na maisha yake, naye ni binadamu, ana familia na wanaomtegemea.
Kaseja ni shujaa wa taifa hili,
kuna rundo la viongozi Yanga na Simba ambao hawajafanya hata robo kama
wataringanishwa naye. Hivyo pia wanapaswa kumpa heshima yake, wahesabu mazuri
yake, ikiwezekana kusahau mabaya aliyofanya kwa kuwa pia ni binadamu.
Kumuwekea Kaseja ubaya ni ubaguzi na
chuki, mkimaliza na Kaseja, mtaingia kwa wachezaji wengine pia na hilo
halitaisha, litadumu na kuwatafuna wengine milele. Kumbukeni jukumu lenu katika
mpira wa Tanzania si kusema maneno ya umbeya.
Siwafundishi, ila najaribu kuwafanya
mfikiri kwamba mnayoyafanya, hayafanani na mnachotakiwa kufanya.
0 COMMENTS:
Post a Comment